Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
TIMU ya madaktari bingwa imeweka kambi ya siku tano katika viwanja vya bustani ya Jiji Februari 17 mpaka 21 mwaka huu kwa ajili ya kutoa huduma ya kibingwa ya tiba mkoba kupitia programu ya “Samia Suluhu Hassan Outrech Service”.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete(JKCL)Dkt.Stella Mongella amesema kuwa tangu kuanza kwa kambi hiyo wamegundua changamoto kubwa ni shinikizo la juu la damu ambalo limebainika kwa wananchi ambapo wengi wao kutojitambua kuwa na maradhi ya moyo na wengine kujitambua .
Dkt.Mongella amesema hayo Februari 20,2025 wakati Akizungumza na waandishi wa habari kuhususiana na timu ya jopo la watalaam nane kutoka Taasisi ya Jakaya kikwete kwa ajili ya kutoa huduma ya kibingwa bobezi ya Magonjwa ya moyo inayojulikana kwa jina la tiba Mkoba (Dkt .Samia Suluhu Hassan)
“Tumefika mkoani Mbeya kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi na mikoa jirani na mpaka sasa tumefikia mikoa zaidi ya 20, hapa nchini na tumeanza kutoa huduma hii kuanzia February 17, na tunategemea kuhitimisha 21, mwaka huu na lengo ya tiba Mkoba ni pamoja na kuleta huduma kwa wananchi na kukuza ushirikiano baina ya Taasisi ya Jakaya kikwete na watoa huduma wenzao wa hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya “amesema Dkt.Mongella.
Hata hivyo Dkt.Mongella amesema kwamba wamefika kuona wagonjwa wenye uhitaji pamoja na watafiti ambao wanakusanya taarifa zinazohusiana na changamoto ya Magonjwa ya moyo ambapo wameweza kuona jumla ya wagonjwa 360, ambapo kati yao ni watu wazima ni 340, na watoto 20, pamoja huku waliohitaji Rufaa ni 34.
“Huduma zingine ambazo tunatoa ni kumuona Daktari ambapo mgonjwa anapimwa urefu, sukari,presha na wenye viashiria vya moyo kufanyiwa uchunguzi na kuandikiwa dawa wanapata vipimo pamoja na kuambatana na madaktari wa mfumo wa lishe”amesema.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Bobezi ya Magonjwa ya moyo kwa watoto,Dkt.Gloria Mbwile ameshukuru serikali kwa kushirikiana na wadau ambao wameandaa kambi hiyo kwa ajili ya uchunguzi wa nagonjwa ya moyo kwa watoto na watu wazima pia kushukuru Taasisi ya moyo ya Jakaya kikwete kwa kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuhudumia wananchi wenye shida ya moyo.
Mmoja wa wakazi wa mkoa wa Njombe aitwaye , Shukran Mgina ambaye amemleta mdogo wake anayesumbuliwa na moyo amesema amefika mkoani Mbeya baada ya kupata Rufaa kutoka hospitali ya Ikonda ambako alikuwa akipatiwa matibabu na mdogo wake kufika katika kambi hiyo.
Aidha Mgina amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwaleta madaftari bingwa mkoani Mbeya ambao wamekuwa msaada mkubwa katika kutoa huduma kwa wananchi kwani baadhi yao walikuwa wanaumwa lakini wengi walikuwa hawajitambui.
“Mdogo wangu amefika hapa na kufanyiwa uchunguzi na kukutwa na tunduma kwenye moyo na mshipa kupasuka kwa hiyo tumeelekezwa kuwa tunapaswa kumpeleka Taasisi ya moyo Jakaya kikwete kwani hapa tulikuja kwa ajili ya uchunguzi tu na tunashukuru tumepata vipimo bila changamoto yeyote “amesema mwananchi huyo.
Kambi hiyo inafanyika katika viwanja vya city Park Jiji Mbeya na kuwa hiyo ni sehemu ya mpango wa Rais Samia Suluhu Hassan Outreach Services”unaolenga kuwafikia wananchi wengi kwa ukaribu Zaidi katika kutoa huduma zaidi kwa afya muhimu.


More Stories
Kamati ya Kudumu ya Bunge yaridhishwa ujenzi soko la Kariakoo
Vitongoji Musoma vijijini vyaendelea kuunganishiwa umeme
Mpango mahsusi wa Taifa kuhusu Nishati wajadiliwa