November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hoteli za kisasa kukuza sekta ya utalii

Na George Mwigulu,TimesMajiraOnline,Katavi.

WAZIRI Mkuu Mstaafu,Mizengo Pinda amepongeza juhudi za wazawa wa mkoa wa Katavi kwa dhamira na maono makubwa ya ujenzi wa hoteli za kisasa ambazo zitatoa mchango mkubwa kwenye kukuza sekta ya utalii mkoani hapo.

Pinda amesema hayo leo katika uwanja wa CCM Azimio Manispaa ya Mpanda wakati wa kufunga maonesho ya siku saba ya wiki ya Mwanakatavi yenye kauli mbiu ya “Katavi yetu talii,wekeza,imarisha uchumi kwa maendeleo endelevu” ambapo sekta za Utalii,Kilimo,Ufugani na Uvuvi ilikuwa ni sehemu ya maonesho hayo.

Amesema kuwa sekta ya utalii nchini inategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa hotel za kisasa zinazokidhi kupokea wageni wa kila aina kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na kuwa kichocheo na kivutio kwao.

Waziri Mkuu Mstaafu akitoa hamasa ya ujenzi wa hotel nyingi za kisasa mkoani Katavi amesema kuwa juhudi zinazofanywa na vijana wa mkoa wa Katavi kujenga hotel nzuri. ” Niwakupongezwa sana kwani ni mwanzo mzuri wa mkoa huo kuwa tayari kukuza utalii kwa maana unazingukwa na vivutio vingi ikiwemo hifadhi ya taifa ya Katavi”

“Tumefanya uzinduzi wa makala ya utalii na tutainadi kila mahali ili watu waone tulichonacho maana jana baada ya kwenda katika Hoteli moja hapa nikaipenda sana ,hivyo nakuagiza Gavana tupige picha hoteli hiyo na tulizo nazo ili tuwaambie wageni kuwa wakija wasiwe na shaka watalala wapi?tupo vizuri sana” Amesema.

Pinda amepongeza ujenzi wa hoteli hiyo yenye hadhi ya nyota tatu na kijana mzawa wa Mkoa huo,Kelvin Mbongo kwa usubutu wake kama kijana kuwekeza kwenye ujenzi wa hotel hiyo ambapo utakuwa sehemu kubwa ya kukuza utalii na kuingiza fedha nyingi za kigeni kwake binafsi na serikali pia hivyo vijana wengi akawaomba kuiga mfano bora kwa kila kijana kuchangamkia fursa.

Mwanamvua Mrindoko,Mkuu wa Mkoa wa Katavi amesema zaidi ya watu 20,000 katika maonesho ya wiki ya Mwanakatavi wamejitokeza kupata mafunzo na ujuzi wa aina mbalimbali kwenye sekta ya utalii,uvuvi,kilimo na mifungo.

Maonesho hayo malengo yake ni kuonesha fursa zinazopatikana katika Mkoa wa Katavi na namna bora za kuzitumia kwa ajili ya maendeleo.

Licha ya kufanikiwa kwenye maonesho hayo na kuyatumia kama sehemu ya kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya mkoa lakini serikali kwa kipindi cha miaka miwili imetoa fedha zaidi ya Bilioni 806 kwenye kuimarisha miundombinu ya afya,elimu,nishati,maji na uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo ni mambo muhimu anayowavutia wawekezaji.

Baadhi ya wadau mbalimbali wakitoa maoni yao ya wiki ya Mwanakatavi.Rashidi Hassain ameipongeza serikali ya mkoa wa Katavi kwa kuwa wabunifu wa kuwa na maonesho hayo ambayo yamekuwa darasa zuri la kukuza maarifa ya kuchangamkia fursa za maendeleo.

Hassain amesema kupitia maonesho ya wiki ya Mwanakatavi wamebaini kunafursa nyingi na wakiwa vijana wananafasi kubwa ya kuzitumia kama vile fursa kwenye sekta za utalii,kilimo na uvuvi wanaweza kuzitumia kukuza uchumi wao.