Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Uyui
SERIKALI imepeleka zaidi ya sh bil 2.5 katika hospitali ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora mwaka huu ili kuboreshwa miundombinu ya afya na kununua vifaa tiba vya kisasa.
Kiasi hicho kimewezesha kujengwa jengo jipya la upasuaji, kuboreshwa jengo la mama na mtoto, kujengwa jengo la kuhifadhia maiti na kuwekwa vifaa tiba vya kisasa katika wodi zote ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa juzi na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt Tumaini Fumbuka alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea Hospitali hiyo ili kujionea kasi ya utekelezaji ilani ya uchaguzi.
Amemshukuru Rais kwa kuwapatia kiasi hicho, kwani kimewaondolea wananchi adha ya kukosa huduma za muhimu, mara nyingi walikuwa wanatumia gharama kubwa kufuata huduma hizo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Ametaja huduma mpya zinazotolewa sasa katika hospitali hiyo kuwa ni pamoja na mionzi (x-ray), ultra sound, mama na mtoto, wagonjwa wa nje (OPD), huduma ya meno, jengo la kufulia, vichomea taka na nyinginezo.
Dkt Fumbuka amebainisha kuwa mbali na kuboreshwa majengo hayo pia wamepokea kiasi kingine kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vipya vitakavyotumiwa na wagonjwa na kufungwa matenki ya kuhifadhia maji.
‘Kuboreshwa kwa miundombinu ya hospitali hii kumerahisisha upatikanaji huduma za afya kwa kwa wananchi na kumewezesha hospitali kutoa huduma zilizo bora ambazo awali hazikuwepo’, amesema .
Mkurungezi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Leokadia Humera amesema mbali na kuboreshwa huduma za afya katika hospitali hiyo pia serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa Mwanamama makini Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imewapatia fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya vituo vya afya na zahanati.
Amesema fedha hizo zimewezesha kuboreshwa huduma za uzazi kwa akinamama na watoto, maabara, upasuaji, utoaji huduma za dharura, mionzi na nyinginezo.
Mkurugenzi amewaeleza wanahabari kuwa hadi sasa vituo vya afya na zahanati zaidi ya 60 zilizojengwa na serikali ya awamu ya 6 katika vijiji mbalimbali katika kipindi cha miaka 2 zinatoa huduma bora kwa wananchi.
‘Tunakupongeza sana mama kwa kazi nzuri unayoendelea kufanya katika wilaya yetu, kama wasaidizi wako tunaahidi kuwa tutaendelea kusimamia ipasavyo fedha zote unazoleta kwa ajili ya utekelezaji miradi ya wananchi’, alisema.
Wakiongea kwa nyakati baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo Mariam Lushu mkazi wa kijiji cha Itobela, Juma Jamal na Asia Moshi wakazi wa Isikizya wamemshukuru Rais Samia kwa kuboresha kwa kiasi kikubwa huduma za afya katika wilaya hiyo.
Wamesema kujengwa kwa hospitali ya wilaya, vituo vya afya na zahanati kumesaidia sana kupunguza kero ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo maeneo mengine.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa