November 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya SDA Pasiansi, kuwekwa Wakfu na Mchungaji Ted, kufanya mkutano CCM Kirumba

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato Ulimwenguni, Mchungaji, Dkt.Ted Wilson anatarajiwa kuiweka Wakfu Hospitali ya SDA Pasiansi iliopo Wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Februari 8,2023.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza,Askofu Mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania , Mchungaji Mark Malekana katika mkutano wa kutoa taarifa juu ya maandalizi ya ujio wa kiongozi huyo, uliofanyika kanisa la SDA Mabatini jijini hapa.

Ameeleza kuwa kwa mwaka huu kiongozi huyo Mkuu kutoka Jimbo kuu la Kanisa lililoko nchini Marekani anafanya ziara Afrika, Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyochaguliwa ambapo atatembelea katika Jimbo La Nyanza Kusini lililopo Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania.

Askofu Malekana, ameeleza kuwa Dkt. Ted Wilson pamoja na mkewe Nancy Wilson wanatarajia kuwasili nchini Tanzania ,Februari 7,2023 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam hivyo watapokelewa na viongozi wakuu wa waumini wa jimbo kuu la kusini mwa Tanzania.

Baada ya hapo Februari 8,2023,atapokelewa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwanza na viongozi wakuu pamoja na waumini wa Jimbo Kuu la Kasikazini mwa Tanzania wakiongozwa na Gwaride maalumu lililoandaliwa na vijana wa kanisa hilo.

“Kiongozi huyu anatarajiwa kuiweka Wakfu Hospitali kubwa ya SDA Pasiansi Mwanza na baadae kuelekea katika uwanja wa CCM Kirumba kukutana na waumini wa kanisa hilo,’JIHUSISHE YESU ANAKUJA’ni kauli mbiu inayobeba ziara hii inayolenga na kusisistiza kila muumini kushiriki kikamilifu katika kazi ya huduma kwa jamii na injili,nawakaribisha wote katika tukio hilo muhimu ili kukutana na kusikiliza ujumbe wa kiongozi wetu,”ameeleza Askofu Malekana.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa siku ya Februari 8,2023 matukio muhimu yatakayofanyika ni pamoja na uimbaji utakaohusisha zaidi ya kwaya ya 150 kutoka mikoa yote hapa nchini, programu za idara za vijana ndani ya kanisa, idara ya wanawake pamoja na hotuba mbalimbali kutoka kwa viongozi hapa nchini pamoja na ya mgeni rasmi Dkt.Ted.

Aidha ametymia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kudumisha umoja,mshikamano na nchi kuwa kisiwa cha amani.

“Tuungane mikono na kiongozi wetu wa nchi Rais Samia katika kuiweka Tanzania kuwa nchi inayopenda amani, mshikamano,msamaha,uhuru,dini zote za madhehebu mbalimbali tuungane kuunga juhudi za viongozi wa taifa kuifanya Tanzania kuwa kisiwa cha amani,”.

Pia ameeleza kuwa haipendezi kuona Mtanzania anarandaranda kutafuta kazi kwani nchi ina fursa katika Kokomo,uvuvi,madini,ufugaji na kila mahali kuna mazao ya kimkakati Kanda ya Magharibi kuna mchikichi,Kanda ya Kati kuna zabibu,alzelti huku Kanda ya Ziwa kuna pamba.

“Watanzania wote tujikite,tufanye kazi kwa ajili ya maendeleo yetu binafsi,familia zetu,ya kanisa na taifa letu,kanisa linawataka watu wafanye kazi nenda ofisini,shambani,biashara na siyo kupata kipato kwa kamali, maandiko yamekataza kabisa maisha ya kubahatisha arukuletea duniani na Mungu kwa kubahatisha halikubaliani na kila aina ya michezo ya kubahatisha,”.

Ikumbukwe kuwa hii ni mara ya tatu kwa Dr Ted Wison kutembelea nchini hapa ambapo kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1988 ambapo alifanya ziara ya kitalii katika Mlima Kilimanjaro,mwaka 2014 alizuru nchini katika jiji la Dar Es Salaam ambapo alifanya mkutano mkubwa wa hamasa ya utume unaojulikana kama “MISSION EXTRAVAGANZA” ambao ulimkutanisha na maelfu ya waumini katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Askofu Mkuu wa Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania , Mchungaji Mark Malekana,akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza hawapo pichani katika mkutano wa kutoa taarifa juu ya maandalizi ya ujio wa kiongozi Mkuu wa kanisa hilo ulimwengu nchini Tanzania, uliofanyika kanisa la SDA Mabatini jijini hapa.