October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya wakutana na Jeshi la zimamoto, Bodaboda, bajaji

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

HOSPITALI ya Rufaa kanda ya Mbeya imekutana na kikosi cha Jeshi la zima Moto na uokoaji,madereva bajaji na bodaboda lengo likiwa ni kutoa elimu ya kukabiliana na wagonjwa wa dharura wawapo katika maeneo yao ya kazi .

Imeelezwa kuwa lengo lingine la kukutanisha makundi hayo ni ni kutoa elimu namna Bora ya kuhudumia na kusafirisha majeruhi wa maafa katika shughuli zao .

Akizungumza kwa niaba na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Mkurugenzi wa Tiba hospitalini hapa Dkt. Uwesu Mchepange amesema makundi hayo waliyoyachagua ni muhimu sana kwa kuwa hospitali ni kituo cha mwisho cha kupokea wagonjwa wa dharura hivyo ni vema kupeleka elimu pia kwa makundi ambayo yanahusika kwa mara ya kwanza pindi mgonjwa anapopata dharura.

Dkt.Mchepange amesema kuwa kuelekea kilele cha siku ya maadhimisho ya Tiba ya magonjwa ya Dharura, wataalamu wa Afya kutoka Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Mei ,24 2024 wamekutana na kikosi cha Jeshi la zimamoto na uokoaji, Madereva Bajaji na Bodaboda lengo ni kutoa elimu juu ya kukabiliana na wagonjwa wa dharura wawapo katika maeneo yao ya kazi.

“Tumewachagua wenzetu hawa wa Jeshi la zima Moto na uokoaji, Bajaji na Bodaboda kwa kuwa wao ni makundi muhimu sana kwa kuwa sisi kama hospitali, timu yetu ya magonjwa ya dharura na ajali inakuwa ni ya mwisho katika kupokea wahanga mbalimbali ikiwemo ajali “amesema Dkt. Mchepange

Dkt. Proper Bashaka, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na ajali amesema mafunzo yaliyotolewa ni ya huduma ya kwanza, Usalama, na namna bora ya usafirishaji wa wagonjwa na majeruhi kutokana na maafa mbalimbali yanayoweza kutokea katika jamii hasa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema kuwa wameandaa mafunzo ya usalama, huduma ya kwanza na namna bora ya usafirishaji wa mgonjwa na majeruhi wanaotokana na maafa mbalimbali ili waweze kufahamu vitu mbalimbali ambavyo wanapaswa kuvifahamu.

Wawakilishi wa makundi hayo yaliyopatiwa mafunzo kutoka Jeshi la Zima moto na Uokoaji , Bodaboda na Bajaji, kwa pamoja wameushukuru uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kwa elimu hiyo waliyopatiwa na kuahidi kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kwa wengine pindi maafa yanapotokea pamoja na kuyafanyia kazi kwa vitendo mafunzo hayo.

“Mafunzo haya tutaenda kuyafanyia kazi kwa vitendo katika maeneo yetu ya kazi ikiwa ni pamoja kuisaidia jamii na watu walio jirani na mazingira yetu ya kazi “wamesema.

Kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya tiba ya Magonjwa ya Dharura inasema “Mabadiliko ya tabia ya nchi ni sehemu ya kiafya ya dharura” ambapo kilele chake kimefanyika Mei 24 ,2024 katika viwanja Kabwe Mkoani Mbeya kikiambatana na utoaji wa huduma mbalimbali bila malipo ikiwemo upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi pamoja na utoaji wa elimu kuhusu huduma ya kwanza.