Na Suleiman Abeid
MWAKA 2020 ni mwaka wa uchaguzi mkuu kwa hapa nchini kwetu ambapo watanzania waliotimiza sifa za kuwa wapiga kura watapata fursa nyingine ya kupiga kura kuwachagua viongozi wao wanaowataka.
Uchaguzi Mkuu unafanyika ikiwa mwaka mmoja umepita tangu pale watanzania walipotumia fursa nyingine ya kuwachagua viongozi wao katika ngazi ya chini ya Serikali za mitaa uchaguzi uliofanyika mwaka jana mnamo mwezi Novemba.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu watanzania watapata tena fursa ya kuwachagua madiwani katika kata zao, wabunge kwenye majimbo yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hii ni baada ya kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2015.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 21 inaeleza kwamba kila raia wa nchi hii anayohaki ya kushiriki anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja moja kwa moja au kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao.
Pamoja na kila raia wa Tanzania kuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi iwe katika ngazi ya Serikali ama kupitia chama chake cha siasa lakini bado kuna kundi la wanawake linashindwa kujitokeza kwa wingi katika kugombea uongozi katika maeneo yao.
Hali hii inasemekana inachangiwa na hofu au kutokujiamini kwa wanawake wengi na hofu ya kulogwa (kufanyiwa vitendo vya kishirikina) japokuwa baadhi yao wanawake wana uwezo mkubwa wa kuongoza ikilinganishwa na uongozi wa wanaume.
Kwa kipindi kirefu kumekuwepo na uhamasishaji wa wanawake kutakiwa kujitokeza kugombea hasa upande wa udiwani na ubunge badala ya wao kukaa kusubiri nafasi za viti vya upendeleo, maarufu kama “Viti maalumu.”
Tunapaswa kuelewa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wananchi ndiyo wenye mamlaka na maamuzi ya watu gani wawachague na kuwaweka madarakani ili waweze kuunda Serikali itakayowaongoza kwa kipindi ambacho kimepangwa ndani ya Katiba ya nchi. (Ibara ya 65 (1) bila kujali jinsi zao.
Kikubwa kinachoangaliwa ni uwezo na utendaji kazi wa mtu anayechaguliwa kuwa mwakilishi wao na mara nyingi kiongozi mwanamke anatajwa kuwajibika zaidi katika utendaji wake ikilinganishwa na mwanamume lakini uwezo huo wanawake wengi hawaoni.
Imekuwa ni kama vile utamaduni uliozoeleka wa kuwahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za udiwani ama ubunge kila kinapofika kipindi cha uchaguzi mkuu hapa nchini, lengo la uhamasishaji huo ni kuwataka wanawake wengi kujitokeza kugombea majimboni.
Japokuwa uhamasishaji hufanyika katika maeneo mengi nchini lakini bado idadi ya ushiriki wa wanawake kwenye kugombea nafasi za uongozi iwe ndani ya vyama vya siasa ama serikalini bado ni ndogo ikilinganishwa na ile ya wanaume hali ambayo inafifisha lengo la uwepo wa 50 kwa 50 katika uongozi wa Umma.
Tukiangalia takwimu za matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hapa nchini mnamo mwaka 2015 utaona wazi jinsi gani ushiriki wa wanawake katika nafasi hizi muhimu za uongozi wa nchini ni wa kiwango cha chini sana na inaonesha wazi bado kazi kubwa ya uhamasishaji inahitajika.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaonesha wagombea wanawake waliojitokeza kugombea nafasi za udiwani kwa mwaka 2015 kwa nchi nzima walikuwa ni asilimia sita pekee (wagombea 670) na asilimia 94 (wagombea 10,046) walikuwa wanaume ambapo nafasi za ubunge majimboni wagombea wanawake walikuwa 233 sawa na asilimia 19 ya wagombea 1,209 waliojitokeza.
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) yalionesha katika wagombea udiwani wanaweka walioshinda kwenye uchaguzi huo walikuwa 204 kati ya madiwani 3,946 walioshinda uchaguzi ambapo kwa upande wa ubunge majimboni wanawake 26 pekee ndiyo walioshinda miongoni mwa wabunge 264 walioshinda katika uchaguzi huo.
Kutokana na matokeo hayo ni muhimu wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu mwingine wa mwaka 2020 kundi hili la wanawake lihamasishwe ili kuwezesha wengi wao kujitokeza kugombea sambamba na wanaume iwe katika nafasi za udiwani ama ubunge na hata nafasi ya juu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baadhi ya wanawake ambao angalao wamekuwa wakithubutu kusimama kugombea majimboni wanasema zipo sababu kadhaa zinazochangia baadhi yao waogope kujitokeza kugombea ikiwemo kutokupata ushirikiano ama kuungwa mkono na wanawake wenzao.
Wanawake hao wanadai mara nyingi kikwazo kwa wale wanaojitokeza kugombea majimboni huwa ni wanawake wenzao kuwadharau na kuwapiga vijembe kwa kudai hawana lolote watakaloweza kulifanya iwapo watachaguliwa kuwa madiwani ama wabunge.
Sili Yasini amaye ni Mwenyekiti wa Mkoa chama cha ACT – Wazalendo mkoani Shinyanga ambaye aliwahi kuchaguliwa kuwa diwani vitimaalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anasema ushirikiano mdogo wa wanawake ni moja ya vikwazo alivyokumbana navyo.
Sili anasema pamoja yeye kujitokeza mara mbili kugombea udiwani katika kata yake ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga hakuweza kuchaguliwa kutokana na kura zake kutokutosha japokuwa wapiga kura wengi katika kata hiyo ni wanawake.
“Mara mbili nagombea katika kata yangu ya Chamaguha kuomba kuchaguliwa kuwa diwani wa kata hiyo lakini sijabahatika kushinda, pamoja na wapiga kura wengi katika kata yetu kuwa ni wanawake lakini mpinzani wangu ambaye ni mwanamume aliniangusha,”
“Kama kweli sisi wanawake tungekuwa na mshikamano wa dhati tungeweza kushinda katika nafasi nyingi tunazojitokeza kugombea, lakini pia kuna changamoto nyingine ya ukereketwa wa vyama vya siasa, hili nalo ni tatizo, wengi pamoja na kuwa na uwezo wa kuongoza tunaangushwa kwa ushabiki wa kivyama,” anaeleza Sili.
Anatoa mfano kwa yeye mwenyewe ambaye pamoja na kujitokeza kugombea udiwani katika kata yake kwa vipindi zaidi ya viwili, lakini bado amekuwa akiangushwa na wapiga kura ambao wengi wao humtaka ahame kwenye chama chake na ajiunge na Chama cha Mapinduzi (CCM) ili wamchague.
Sili anasema ifike sehemu wanawake waache kuzubaishwa na nafasi za upendeleo na kwamba kwa wale ambao tayari wamepata fursa ya kuchaguliwa kuwa diwani au mbunge wa vitimaalumu hawana sababu za kukaa kwenye nafasi hizo kwa zaidi ya kipindi kimoja.
“Unajua wanawake wengi tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendeshea kampeni, lakini kwa yule anayepata nafasi ya kuchaguliwa kwenye vitimaalumu, miaka mitano ya uongozi wake inamtosha kupata fedha, hivyo atoke huko na aende kugombea kwenye kata ama jimboni,”
“Wengi tunaweza kushinda katika maeneo tunayogombea iwapo tutashikamana na kuwa na umoja, na tuache kupigana vijembe, maana anaposimama mwanamke kugombea dhidi ya mwanamume, badala ya wenzake kumuunga mkono, wao ndiyo wanakimbilia kwa mgombea mwanamume kuwa mameneja kampeni wake,” anaeleza Sili.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga, Winfrida Rwehumbiza anasema changamoto nyingine inayochangia wanawake wengi waogope kujitokeza kugombea nafasi za udiwani ama ubunge ni uwepo wa dhana ya ushirikina wakiamini wakijitokeza kutaka kugombea watalogwa.
Winfrida anasema hofu ya mtu kulogwa ni moja ya kikwazo kinachochangia wanawake wengi wasijitokeza kugombea majimboni ambapo anasema hofu hiyo hupata nguvu pale inapotokea mmoja wa mgombea anapopatwa na tatizo lolote la kiafya huhisiwa amelogwa na wapinzani wake.
“Nafikiri hizi kampeni na hamasa za kila miaka za kutuhamasisha sisi wanawake ili ziweze kufanikiwa na kuwa na matokeo mazuri ni vizuri pafanyike marekebisho kwenye sheria za uchaguzi, Katiba za vyama vya siasa na Katiba mama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pawekwe utaratibu mzuri utakaowezesha wanawake kugombea,” anaeleza Winfrida.
Winfrida pia anaungana na kauli ya Sili kwamba ukereketwa wa uliopitiliza wa vyama vya siasa kwa baadhi ya wanawake n ahata wanaume ni kikwazo cha wanawake wengi kutochaguliwa katika maeneo yao hata kama watakuwa wamethubutu kujitokeza kugombea.
Anasema baadhi ya wanawake wengi wanaamini kuwa ili uweze kuwa kiongozi iwe kwenye ngazi ya Serikali za mitaa, udiwani na ubunge lazima utokane na Chama Tawala CCM na kwamba baadhi ya wanawake wenye uwezo mkubwa wa kuongoza kuliko hata wanaume wanashindwa kujitokeza kwa vile hawataki kugombea kupitia CCM.
Erenestina Richard ambaye ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga vijijini anasema zipo changamoto nyingi zinazochangia wanawake wengi washindwe kujitokeza kugombea katika nafasi za majimbo na hivyo kusubiri nafasi za vitimaalumu.
Anasema moja ya changamoto kubwa ni wivu miongoni mwa wanawake wenyewe kwa wenyewe hali inayochangia washindwe kumuunga mkono mwanamke mwenzao pale anapojitokeza kupambana na mgombea mwanamume.
“Hii hali imo mpaka ndani ya vyama vyetu vya siasa, sisi wanawake bado tuna changamoto ya kutopendana, mara nyingi tuko tayari kuwaunga mkono wagombea wanaume kuliko wanawake wenzetu, na hili si jingine bali ni wivu tu, kwani huyu apate, akichaguliwa atalinga,”
“Naamini kama sisi wanawake tukishikamana na kuondoa tofauti zetu, tukawa kitu kimoja kata nyingi ama majimbo ya ubunge yataongozwa na madiwani au wabunge wanawake na itafika wakati hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atachaguliwa mwanamke, maana wapiga kura wengi ni wanawake,” anaeleza Erenestina.
More Stories
Mussa: Natamani kuendelea na masomo,nikipata shule ya bweni
Tanzania inavyowahitaji viongozi wanawake aina ya Mwakagenda kuharakisha maendeleo
SCF inavyotambua jitihada za RaisSamia mapambano dhidi ya saratani