November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hizi ndio sababu za Rais Magufuli kumtumbua aliyekuwa Mkurugenzi NIMR

Na Penina Malundo

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameweka bayana sababu ya  kumtumbua aliyekuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR).

Akizungumzia leo mkoani Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Rais Magufuli amesema mkurugenzi huyo alitumika kutangaza kuwa Tanzania imekumbwa na ugonjwa wa Zika jambo ambalo si kweli ambapo hadi leo ugonjwa huo haupo nchini.

Amesema baada ya kumfukuza  waliomtuma kusema hayo wakamteua kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika ambapo mpaka leo miaka karibu mitano hapajawahi kuwa na kesi ya Zika nchini.

“Nilipoingia madaraka tuliambiwa Tanzania kuna ugonjwa unaoitwa Zika, aliyetumiwa kutangaza nikamfukuza kazi na bahati mbaya ni mgogo, hata hivyo siku chache baadae akateuliwa na watu waliomtuma atangaze kuwa tuna Zika,” amesema na kuongeza

” Baada ya kumfukuza yule Mgogo waliomtuma wakamteua kuwa Mkurugenzi, mpaka leo miaka karibu mitano hapajawahi kuwa na kesi ya Zika hapa Tanzania,”anasema

Anasema  baada ya uzushi wa Zika kupita na kumfukuza  kazi aliyesema kuna Zika, tukakaa baadaye tukaambiwa kuna ugonjwa wa Ebola na hii walijua wakisema ugonjwa wa  Ebola upo nchini watalii hawatokuja.

“Tukasema sisi hatuna Ebola, wala mjukuu wake Ebola, hatujaona mgonjwa amekufa na Ebola, hilo nalo likapita,” amesema  Aidha amesema sasa  umekuja ugonjwa wa Corona ambao baadhi ya watu walilitabiria Bara la Afrika litapoteza raia wake wengi na maiti zitazaa barabarani.

Disemba 16, 2016 aliyekuwa Mkurugenzi wa NIMR, alitangaza kugundulika kwa virusi vya Zika  nchini, kufuatia hatua hiyo Rais Magufuli alitangaza kumtumbua mkurugenizi huyo. Hata hivyo Aprili 8, 2018 Dk. Mwele aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO wa kanda ya Afrika.