Na Lubango Mleka, Timesmajiraonline,Tabora
KILA Mwaka ifikapo Juni 16 Tanzania huungana na Mataifa mengine Barani Afrika kuadhimisha siku ya Mtoto wa Afrika.
Chimbuko la maadhimio ya Siku ya Mtoto wa Afrika liliridhiwa na uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka maelfu ya watoto waliouawa kwenye maandamano mjini Soweto nchini Afrika Kusini 16 Juni.1976.
Watoto hao waliuawa wakati wa mapambano ya utawala wa weupe wachache (makaburu) waliyoitawala nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika kwa karne nyingi.
Maelfu ya watoto waliandama kwa ajili ya kudai haki zao za msingi kama vile afya bora na elimu bora, Askari wa Serikali ya Kikaburu waliwafyatulia risasi waandamanaji hao ambapo mamia ya watoto waliuawa na maelfu wengine kujeruhiwa.
Lengo mahususi ya maadhimisho hayo ni kuenzi mchango wa watoto hao walioshiriki katika maandamano ikiwa ni pamoja na kuijengea jamii kuelewa umuhimu wa kuwapatia elimu bora watoto.
Tanzania ikiwa ni moja ya nchi mwanachama wa AU iliungana na mataifa mengine kuadhimisho siku hiyo adhimu.
Maadhimisho hayo yalifanyika nchi nzima ikiwemo wilayani Igunga mkoani Tabora katika kiwanja cha kumbukumbu ya Sokoine kilichopo Mamlaka ya mji mdogo wa Igunga ambapo zaidi ya watoto 1500 kutoka shule mbalimbali za Msingi, Sekondari na Wasiosoma walihudhuria maadhimisho hayo.
Akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga, Joseph Mafuru, wanatumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania, hususani katika kusimamia masula yote yanayohusu ustawi wa watoto na kupinga ukatili wa watoto katika wilaya ya Igunga.
“Pia nichukue nafasi hii kuzipongeza idara zote za Serikali ikiwemo Dawati la jinsia Polisi, ustawi wa jamii, SMAUJATA, Wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla kwa kuendelea kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto katika wilaya yetu,” anasema Mafuru.
Anaendelea kusema kuwa; “Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya ukatili wa watoto mtandaoni (Disrupting Harm Report in Tanzania 2022) inaonesha kuwa katika kila nchi duniani watoto ndio kundi linaloongoza kwa utumiaji wa bidhaa za mawasiliano zikiwemo simu janja, kopyuta na intaneti, ambapo nchini Tanzania asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 -17 hutumia mitandao ikiwemo simu na intaneti. “
“Watoto hao hutumia simu za ndugu zao wa karibu wakiwemo wazazi, walezi, marafiki na ndugu wengine wanaowazunguka.
Pia taarifa hiyo inaeleza kuwa asilimia nne ya watoto ni wahanga wa aina mojawapo ya ukatili wa mitandaoni ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya kingono, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao, aidha hurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi zingine. “
Aidha, anasema kuwa katika kukabiliana na changamoto zinazohusu ukatili na ukiukwaji wa haki za watoto, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imefanya jitihada ya kuridhia na kusaini mikataba ya kimataifa kuhusu haki za mtoto mwaka 1991, na mkataba wa Afrika wa haki na ustawi wa mtoto wa mwaka 2003 ambayo yote kwa pamoja imetoa miongozo ya kusimamia ulinzi na haki kwa mtoto.
“Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2004 na kutunga sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na kufanyiwa marekebisho kwenye baadhi ya vifungu vya sheria ya Elimu ya mwaka 1978 kwa kuongeza kipengele kinachotoa adhabu ya kifungo cha hadi miaka 30 kwa mtu yoyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi au kuhusika katika kukatisha masomo yake, ” alisema Mafuru.
Anaongeza kusema kuwa, Halmashauri ya Igunga kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii imekuwa ikiwezesha vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mikopo isiyo na riba ili kuwainua kiuchumi na pia imekuwa ikiwezesha kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuwawezesha kiuchumi.
Na hii yote ni kufanya kila jitihada kuondoa malezi hafifu na ukatili kwa watoto, kwani wanaamini mtu akijitegemea kiuchumi ndio ataweza kuwasomesha watoto na kuwapatia mahitaji yote ya msingi kwa ustawi wake.
Katika kuimalisha ulinzi wa mtoto katika ngazi za mikoa na wilaya, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeanzisha Dawati la Jinsia na Watoto katika vituo vya Polisi nchini kwa lengo la kupokea taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe, na pia imefanikiwa kuanzisha Mahakama za kusikiliza mashauri ya watoto kila wilaya nchini na halmashauri imesimamia uanzishwaji wa mabaraza ya watoto.
Mbali na hayo bado Serikali imefanya jitihada za kuandaa nyenzo mbalimbali kwa ajili ya kuelimisha watoto, wazazi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu ukatili wa watoto mitandaoni.
Nyenzo hizo ni pamoja na vitini maalumu vinavyoeleza namna watoto wenyewe wanavoweza kujilinda na ukatili, lakini pia wazazi wanavyoweza kuwalinda watoto na kuwafanya wawe salama wakati wanapotumia mitandao.
“Pia Serikali yetu imeratibu uanzishwaji wa namba ya bure ya simu kwa lengo la kutoa taarifa za vitendo vya ukatili, namba hiyo ni 116 na inawasaidia wahanga na wadau wengine kutoa taarifa pindi wanapohisi au ukatili unapofanyika na kuhitaji msaada wa haraka, unapopiga namba hii ni bure na ni kwa mitandao yote nchini, ” alisema Mafuru.
Hata hivyo Mafuru alieleza utatuzi wa baadhi ya changamoto zilizosomwa katika risala na afisa ustawi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Nuru Kasote, kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wahanga wa ukatili na watoto, kuendelea kutoa elimu katika ngazi ya jamii ili kupunguza vitendo vya ukatili kwa watoto.
“Tunaomba kuongezewa maofisa wa ustawi wa jamii pale ajira zinapotoka, kujipanga kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga nyumba maalumu kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga wa ukatili.” Anasema Mafuru.
Mafuru ametoa wito kwa wazazi, walezi, na wadau wote wa makuzi na malezi ya watoto kuhakikisha wanazingatia kuwa watoto wajiepushe kwenda kwenye maeneo ambayo ni hatari kwa usalama wao kwani wanaweza kushawishiwa kufanya ngono, kubakwa, kulawitiwa na hata kuuwawa.
“Wazazi au Walezi muwaruhusu watoto kushiriki katika mabaraza ya watoto na klabu za watoto shuleni, kwani husaidia kujenga uwezo wa mtoto katika kufikiri, kujiamini na kujieleza, hakikisheni watoto hawatumii vifaa vya kielektroniki kama simu, intanenti na luninga bila ya uangalizi wa karibubu ili kumwepusha mtoto kujiingiza kwenye maeneo hatari ya kuweza kufanyiwa ukatili wa mtandaoni, “
“Pia matumizi yaliyopita kiasi yanaweza kusababisha uraibu kwa mtoto, na athari zake ni pamoja na kukosa muda wa kujisomea na kusaidia kazi za nyumbani, pia hakikisheni watoto hawafanyi kazi hatarishi, kwani sheria inatoa zuio kwa watoto kuajiriwa migodini, vyombo vya majini (Melini), viwandani na kwenye mashamba makubwa, na ni kinyume na sheria ya mtoto kuwa kwenye baa, vilabu vya pombe na kumbi za sherehe hasa nyakati za usiku.
Mafuru anaendelea kusema kuwa, watoto, wazazi au Walezi wanatakiwa kutoa taarifa ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kwenye dawati la jinsia la watoto kwenye vituo vya Polisi ili kutoa msaada, Maofisa maendeleo na ustawi wa jamii na wadau wengine katika wilaya yetu waimalishe utoaji wa Elimu ya malezi na makuzi ya watoto kwa wazazi na walezi ili waelewe wajibu wao wa kulea watoto kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa wa kijinsia.
“Watoto waelekezwe kutimiza wajibu wao wa kuwaheshimu wazazi, walimu na wanajamii wote, pia kufanyanyia kazi maelekezo wanayopewa ili kuwa salama kwa ustawi na maendeleo, hivyo niwaombe viongozi wote wa Serikali, Dini, Madiwani na viongizi wa vyama vya siasa kuendelea kusimamia na kutoa elimu ya malezi na makuzi mema ya watoto wetu, “
“Wazazi tuhakikishe tunashirikiana na walimu katika hakikisha watoto wote wanaotakiwa kwenda shule wanakwenda na wanasoma hadi wanahitimu masomo yao, kwani kauli mbiu ya mwaka huu inasema;
“Elimu Jumuishi kwa Watoto: Izingatie Maarifa, Maadili na Stadi za Kazi.” Kauli mbiu hii inahimiza utoaji wa elimu inayojumuisha watoto wote, isiyobagua mtoto kutokana na hali yake, “
“Aidha, elimu hiyo ilenge kumpatia mtoto maarifa (elimu bora na ufaulu) , maadili (yaani maadili mema, uadilifu na hofu ya Mungu) na stadi za kazi (kazi za mikono ili kujenga ujuzi kulingana na umri wa mtoto), ” alimaliza kusema Mafuru.
Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii halmashauri ya wilaya ya Igunga Nuru Kasote amesema kuwa Siku hii ya Mtoto wa Afrika hutoa furusa kwa wadau mbalimbali wa kupinga ukatili na haki ya mtoto kujadili mambo yanayowakabili watoto.
“Kupitia maadhimisho haya Serikali na wadau wengine tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza uelewa wa wazazi na jamii kujua changamoto zinazowakumba watoto wa Afrika, aidha tunakumbushwa pia sera zinazoandaliwa na serikali zinazohusu watoto kwa kuwapatia huduma staiki za Afya, Elimu, Ulinzi na Malezi bora ili kuwalithisha stadi za maisha na tunu ikiwemo Utu, uzalendo, uadilifu umoja, uwazi, uwajibikaji na lugha ya taifa kwa manufa ya familia na taifa kwa ujumla,” alisema Nuru.
Huku, Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Polisi Igunga Fortuna Sanga, akibainisha changamoto zinazowakumba watoto wa Igunga kuwa ni pamoja na baadhi ya watoto kutokwenda shule kama sheria inavyo taka, watoto kuozeshwa na wengine kukatishwa masomo na kwenda kuchunga ng’ombe kutokana na kuwepo kwa jamii za kifugaji zinazoendekeza mila zinazokandamiza haki za watoto.
” Kwa hapa mjini Igunga sio sana jamii kutowapatia elimu watoto ila kwa pembezoni mwa mji na vijijini kuna wimbi kubwa la watoto kutokwenda shule kwa sababu ya kuchunga au kuozeshwa katika umri mdogo kwa hiyo sisi kama watendaji wa Serikali tuna kazi kubwa sana ya kuwakomboa watoto hawa, pia bado hapa Igunga kuna watoto wa kike wanafanyiwa ukeketaji hasa katika jamii ya kitaturu iliyopo pembezoni mwa wilaya yetu bado wanakeketa watoto kwa siri sana, ” alisema Sanga.
Aliendelea kwa kusema kuwa, bado kuna wimbi kubwa la watoto kubakwa na kulawitiwa kwa wilaya ya Igunga, ambapo watoto wana lawitiana mashuleni, majumbani, na hata wazazi wa kufikia wanawabaka watoto wa kike na kuwalawiti wa kiume.
“Ninaiomba jamii ya watanzania kutusaidia kufichua matukio haya ya unyanyasaji wa watoto na matukio mengine ya kijinsia, ili tuweze kuwa kamata wahusika na kuwachukulia sheria ili iwe fundisho na matukio haya kuyakomesha katika wilaya yetu na kwa taifa zima, ” alisema Sanga.
” Sisi kama SMAUJATA wilaya ya Igunga tunashirikiana na Serikali kutoa elimu Makanisani, Misikitini, Minadani, Shuleni na katika mikusanyiko mingine kama hiyo juu ya haki za mtoto na kupinga ukatili wa kijinsia, rai yangu tu kwa mashirika au taaasi ambazo zinakwenda kinyume na maadili ya nchi yetu tunawaambia hatutakubali watoto wetu, wadogo zetu na kaka na dada zetu kufanya mambo ya hovyo kwa sababu ya matakwa ya taasisi au mashirika hayo na tuanawaambia kuacha mara moja na waondike tu wenye nchini kabla hatujawachukulia hatua za kisheria, ” alisema Mwenyekiti wa SMAUJATA Igunga Charles Masi.
Kwa upande wao baadhi ya watoto wilayani hapa waliojitambulisha kwa majina ya Baraka Samwel (11) mwanafunzi wa Shule ya msingi Igunga, Charles Samwel (13) mwanafunzi shule ya msingi Buyumba, Joyce Emannuel (15) kutoka Sekondari ya Mwayunge, Jumanne Ramadhani (15) kutoka Sekondari ya Kamando na Monica Mipawa (16) kutoka Shule ya Sekondari Hanihani wanatoa shuhuda ya changamoto wanazokutana nazo.
Wanaeleza badhi ya changamoto zinazowakabili wanafunzi na watoto wa kike kuwa bado baadhi ya madereva bodaboda, bajaji na madereva wa magari ya abilia (hiace) kuwataka watoto wa shule kimapenzi na wanapo wakatalia huwadharirisha utu wao kwa kuwatolea matusi na kuwakashifu.
“Kuna baadhi ya wanafunzi wenzetu ambao wanatokea kijiji cha Makomelo ambao wanakuja hapa shuleni kwetu Hanihani Sekondari kupata elimu, kutokana na umbali na wazazi kutokuwa na uwezo wamekuwa wakikumbana na changamoto ya usafiri na wanapopatiwa rifti basi madereva huwataka kimapenzi.
Na wanapogoma hutukanwa na hata kushushwa kwenye magari jambo hili limekuwa likiwakatisha tamaa hata ya kusoma na wengine kuacha shule, ” anasema Monica
Jumanne Ramadhani kwa upande wake ameiomba Serikali kuanzisha madawati ya jinsia kuanzia ngazi ya vijiji, vitongoji hadi kata na si wilayani pekee, jambo ambalo litasaidia kutokomeza na kuwabaini mapema watu wote ambao wanafanya ukatili wa kijinsia na kukandamiza haki za watoto.
“Kuna wananchi wanapenda kufichua wahalifu wanaokandamiza haki za mtoto na kufanya ukatili wa kijinsia ila sasa wanashindwa kwa sababu vyombo husika vipo wilayani na wengine wanogopa kwenda Polisi kutoa ushahidi kwa sababu ya hofu ya kutolewa siri zao kwa wahalifu.
Hivyo niiombe wadau kuunga juhudu za Rais Samia za kupinga ukatili na kutetea haki za mtoto ikiwemo kuanzisha madawati ya jinsia kuanzia ngazi za vijiji hadi kata na si kuishia wilayani pekee.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika