December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Historia yaandikwa Papa Francis, Rais Samia Vaticam

Na Mwandishi Wetu

RAIS Samia Suluhu Hassan, jana Februali 11, mwaka huu ameanza ziara yake Vatican kwa mwaliko wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis .

Papa Francis alimpokea Rais Samia mara baada ya kuhudhuria misa takatifu katika Kanisa la Mtakatifu Peter (St Peter’s Basilica.

Ziara hiyo itakuwa ya siku mbili, yaani Februari 11 na 12 na Febrauri 13 Rais atawasili Norway kwa ziara nyingine ya siku mbili.

Jana, Februari 11, 2024, ambayo ilikuwa siku ya maadhimisho ya miaka 95 ya uhuru wa Dola ya Vatican. Februari 11, 1929, aliyekuwa Mfalme wa Italia, Victor Emmanuel III na Papa Pius XI, walisaini Mkataba wa Lateran, ulioitambua Vatican kuwa ni Kiti Kitakatifu (The Holy See).

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, Rais Samia akiwa Vatican, atakuwa na mazungumzo na Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na Katibu wa Vatican, Pietro Parolin.

Alisema uhusiano kati ya Tanzania na Vatican ulianza miaka ya 1960 wakati ambapo Vatican ilianzisha Ubalozi wake hapa nchini.

Tangu wakati huo Vatican kupitia Kanisa Katoliki imekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha na masuala ya kiroho, amani, elimu na program za afya.

Kwenye ziara hiyo Rais Samia ataongozana na wawakilishi watano wa waumini wa Kanisa Katoliki Tanzania kutoka kwenye jumuiya mbalimbali za kanisa hilo.

“Vatican kupitia Kanisa Katoliki limechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu kabla na baada ya uhuru wa Tanzania Bara kwa kutoa elimu kwa Watanzania wa dini zote.

Rais Samia Suluhu Hassan

Kupitia shule na vyuo mbalimbali Kanisa kwa kushirikiana na Serikali limechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha viongozi na wataalam mahiri kwenye maeneo mbalimbali,” alieleza Makamba na kuongeza;

“Kanisa Katoliki linakadiriwa kumiliki zaidi ya shule za chekechea 240, shule za msingi 147, shule za sekondari 245, vyuo vya ufundi 110, vyuo vikuu 5 na taasisi za afya 473 zikiendeshwa na Kanisa Katoliki.”