Na Yeremias Ngerangera,TimesMajira Online. Namtumbo
HIFADHI ya Taifa ya Nyerere, imeanza kuandaa mpango wa jumla wa usimamizi wa hifadhi kwa lengo la kusimamia uhifadhi endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Hifadhi, Stephano Msumi katika barua yake ya Oktoba mwaka huu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, katika kufanikisha mpango huo wameunda kikundi kazi ambacho kitakusanya maoni ya wadau ambayo yatajumuishwa kwenye mpango huo.
Msumi amesema kikundi kazi hicho, kitaanza kutembelea wadau kwa muda wa siku tano, kuanzia juzi hadi Ijumaa kwa lengo la kupata maoni kuhusu ya utengenezaji wa mpango wa uhifadhi endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo.
Hata hivyo Msumi katika mpango huo, awali amewataja Maofisa wanaoshughulikia utalii, wanyamapori, mipango, maendeleo ya jamii pamoja na ardhi kuwa watakuwa wadau wa kwanza kuingizwa katika majadiliano hayo.
Kwa upande wake Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Ernest Nombo amesema mpango huo utasaidia kuwa na uhifadhi endelevu, lakini pia Hifadhi ya Taifa ya Nyerere itasaidia halmashauri katika kutoa elimu kwa jamaii kuhusu umuhimu wa uhifadhi.
Nombo amesema wananchi wa Wilaya ya Namtumbo, utalii ni kitu kipya hivyo kupitia uanzishwaji wa uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere wakazi wilayani hapa, watafahamu umuhimu wa uhifadhi na kutembelea vivutio vya kiutalii.
More Stories
Bei za mafuta Novemba 2024,zaendelea Kushuka
TARURA yaomba Mkandarasi aitwe
Ilemela yakusanya bilioni 3.7.robo ya kwanza