Fresha Kinasa, TimesMajira Online Mara.
JAMII imehimizwa kuendelea kutambua na kuthamini kwa dhati mchango mkubwa wa kimaendeleo unaotolewa na Wanawake katika nyanja mbalimbali hapa nchini.
Afisa Uhamasishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na Mapambano ya ukatili wa Kijinsia mkoa wa Mara Emmanuel Gudluck,ameyasema hayo Machi 8, 2025 wakati akizungumza na Timesmajira katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Wilayani Tarime Mkoani Mara.
Maadhimisho hayo kimkoa yamefanyika Wilayani humo, ambapo yamewaleta pamoja Wadau mbalimbali kutoka Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali, Taasisi za Umma, Elimu na Viongozi wa vyama vya Siasa. Ambapo kauli mbiu kwa mwaka huu inasema,’Wanawake na Wasichana 2025 tuimarishe haki,usawa na uwezeshaji’
Good luck amesema, mchango wa Wanawake hapa nchini katika masuala mbalimbali unapaswa uthaminiwe na kila mmoja kwani wamekuwa wakifanya vizuri katika masuala ya uongozi, uzalishaji,ushauri na malezi ambayo yanamchango mkubwa katika kuimarisha kizazi chenye maadili na mshikamano kwa faida ya Jamii na Taifa pia.
“Tuthamini mchango wao katika kusukuma mbele maendeleo ya Jamii na Taifa letu, wapo Wanawake Viongozi serikalini wanafanya kazi nzuri katika uongozi kinara ni Rais wetu Dkt.Samia Hassan, wapo katika Vyombo vya Habari wanafanya kazi nzuri ya kuibua kero na kuelimisha Jamii idara zingine nyingi. Na pia katika jukumu la malezi wamekuwa mstari wa mbele kulea watoto na kufanya shughuli za uzalishaji mali ikiwemo biashara na familia nyingi wamekuwa nguzo muhimu na tegemeo.” amesema Good luck.
Ameongeza kuwa, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania kupitia Mkurugenzi wake Rhobi Samwelly litaendelea kutoa elimu kwa Jamii na kupinga ukatili dhidi ya Wanawake na watoto Mkoani humo na kuwaunga mkono katika juhudi zao za maendeleo kwa faida ya Jamii.
“Kuna baadhi ya maeneno ndani ya Mkoa wetu wanawake wanakosa fursa ya kumiliki mali mfano kama amefiwa mume kutokana na mila kandamizi, lazima elimu itolewe kwa Jamii izidi kutambua thamani yao na kuongeza wigo wa sauti yao kusikika katika majukwaa mbalimbali ili kuleta usawa. Lakini pia wanaume wasijione wanyonge wanapofanyiwa ukatili na wake zao watoe taarifa lengo ni kuleta usawa wenye tija kwa maendeleo.”amesema Good luck.
“Mfano mzuri ni Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania Rhobi Samwelly, amekuwa msaada mkubwa kupitia Nyumba Salama anazozisimamia zinazohifadhi mabinti wanaokimbia ukeketaji, ameonesha uwezo mkubwa na upendo kwa kuwapa huduma zote muhimu mabinti, pia kuwaendeleza kitaaluma ili watimize ndoto zao huyo ni mwanamke mchango wake katika Jamii unaonekana.” amesema Jesca Marwa Mkazi wa Nyandoto Wilaya ya Tarime.
Naomy Mwita ni Mkazi wa kata ya Bomani Wilaya ya Tarime ameiambia Timesmajira kuwa, Wanawake wanayonafasi kubwa ya kuendelea kuleta mabadiliko katika Jamii iwapo watapewa fursa na kuaminiwa kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika mwaka huu akidai uwezo wao ni mzuri katika kushughulikia kero za Wananchi kwa wakati.
Aidha, Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limetunukiwa cheti cha pongezi na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kupitia Ofisi ya Maendeleo ya Jamii ikiwa ni kutambua mchango wa shirika hilo katika mapambano ya ukatili wa Kijinsia Wilayani humo na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

More Stories
Changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza kuathiri ustawi wa familia,watoto
Watanzania wahimizwa kulinda,kuenzi utamaduni
Rais Samia :Tanzania ni msimamizi mpango wa nishati safi Afrika