Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji, Geoffrey Mwambe amesema serikali imedhamiria kuendeleza eneo la Bagamoyo lenye ukubwa wa hekta 9,800, kwa ajili ya uendelezaji wa mradi wa Eneo Maalum la Kiuchumi Bagamoyo.
“Eneo hilo sio mradi wa Bandari ya Bagamoyo peke yake bali mradi wa Bandari ni miongoni mwa miradi zaidi ya sita itakayotekelezwa kwa pamoja, ikiwepo miradi ya maeneo maalum ya Viwanda, Uendelezaji wa Teknolojia, Taasisi za Utafiti masuala ya viwanda na Biashara, Taasisi za Elimu, Usafirishaji na Utunzaji wa Bidhaa, Uendelezaji makazi, Huduma za jamii na Utalii”
Waziri Mwambe ameyasema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa mradi huo, leo tarehe 17 Novemba, Jijini Dar es salaam, ambapo amebainisha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa nyakati tofauti amabainisha dhamira yake ya kufufua majadiliano ya mradi huo. Hivyo kwa sasa serikali imekamilisha maandalizi ya majadiliano na wawekezaji.
Amebainisha kuwa kati ya hekta 9,800 zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo, hekta 3,000 ndizo zitakazojadiliwa kwa ajili ya uwekezaji wa Bandari ya Bagamoyo kati ya serikali ya Tanzania na wawekezaji wa China na Oman. Aidha, ameongeza kuwa Hekta 6,800 zilizobaki tayari hekta 2,600 zimelipiwa fidia kwa ajili ya uwekezaji na Mamlaka ya Bandari, COSTECH, EPZA na Taasisi ya Uongozi Institute.
Ameongeza kuwa hekta 3,000 za mradi huo,majadiliano yanaendelea ambapo, Kampuni ya China Merchants Holdings na Mfuko wa Uwekezaji wa Serikali ya Oman, wamepanga kuendeleza eneo hilo kwa kujenga Bandari ya Bagamoyo, Kituo cha Usafirishaji kwenye eneo la hekta 800 na uemdelezaji wa eneo Maalum la viwanda kwenye hekta, 2,200 ambapo uwekezaji huo unakadiriwa kufikia Dola za kimarekani milioni 3,100.
Aidha, Waziri Mwambe ametoa wito kwa wewekezaji kuwekeza kwenye eneo hilo maaluum la uwekezaji huku akisisitiza hata wamiliki wa sehemu ya ardhi ya eneo hilo serikali ipo tayari wao wenyewe kuwekeza viwanda katika maeneo hayo badala ya kuwalipa fidia na baadae wapewe maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.
Akizitaja faida za mradi huo, amefafanua kuwa ni kuifanya Bandari ya Dar es salaam kupata mbadala wake hivyo utasaidia kuongezeka kwa biashara ya usafiri baharini na hivyo kukua biasha ya Mamlaka ya Bandari. Pia amesema ajira zitapatikana, ukuaji wa uchumi hususani kwa wakazi wa Bagamoyo lakini nchi mapato yataongezeka.
Amesisitiza kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu- uwekezaji tayari imefanya tathmini ya mradi na kuendeleza majadiliano, ambapo wawakilishi wa serikali wanashiriki kikamilifu kuhakikisha wanasimamaia mazungumzo hayo kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
More Stories
Madiwani Ilala watoa chakula kwa watoto yatima
Waziri Mkuu: Tumieni matokeo ya tafiti za kisayansi katika utekelezaji wa mipango ya kitaifa
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano