May 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hatifungani ya kwanza yazinduliwa iTrust

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya itrust finance limited imezindua rasmi hatifungani yake ikiwa ni hatifungani ya kwanza nchini kutolewa na kampuni wakala wa soko la hisa na msimamizi wa mifuko ya uwekezaji nchini tanzania.

Hatifungani hii ni ya muda wa kati (medium-term note programme) yenye thamani ya shilingi bilioni 100.

Akizungumza katika uzinduzi huo Afisa mtendaji mkuu wa iTrust Finance Limited Faiz Arab alisema kuwa awamu ya kwanza ya program inalenga kukusanya shilingi bilioni 15 ikiwa na nyongeza ya shilingi bilioni 5 kupitia chaguo la ziada.

wawekezaji wanatarajiwa kupata riba shindani ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mine,anasema

Alisema kuwa riba ya hatifungani hiyo italipwa kila baada ya miezi mitatu bila kukatwa kodi (withholding tax) jambo linalolenga kuwapa wawekezaji mapato ya uhakika na yanayotabirika.

Muundo wa hatifungani hiyo umeandaliwa kwa namna inayowavutia wawekezaji wa aina mbalimbali huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa shilingi 500,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji binafsi na taasisi kushiriki kwa urahisi.

Hatifungani hiyo ina manufaa mbalimbali ikiwemo riba shindani yenye kiwango kisichobadilika msamaha wa kodi ya zuio kwenye riba pamoja na kuongeza fursa ya uwekezaji kupitia dhamana za mapato yasiyobadilika (fixed income investments).

Aliongeza kuwa muda mfupi wa ukomavu wa miaka minne pamoja na mfumo wa malipo ya kila robo mwaka vinaifanya itrust bond kuwa mbadala wenye mvuto ukilinganishwa na dhamana za kawaida za serikali.

fedha zitakazopatikana kupitia utoaji wa hatifungani hiyo zitatumika katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kuongeza uwezo wa utoaji mikopo, kuwekeza katika majukwaa ya kidijitali ya kisasa pamoja na kuimarisha mtaji wa uendeshaji wa kampuni kwa ajili ya kukuza shughuli zake,

Katika kurahisisha usajili wa itrust bond namna rahisi ya kuwekeza kupitia uzinduzi wa programu ya simu ya itrust app.

Programu hiyo ya kipekee itawawezesha watumiaji kuwekeza katika hatifungani, hisa na mifuko ya uwekezaji huku wakifuatilia uwekezaji wao wote katika sehemu moja.

iTrust finance limited ni taasisi ya huduma za kifedha ya daraja la pili (tier 2) iliyoidhinishwa na kusimamiwa na benki kuu ya tanzania (bot) pamoja na cmsa.

Kampuni hiyo hutoa huduma mbalimbali za kifedha zikiwemo uwakala wa soko la hisa, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mifuko ya uwekezaji pamoja na huduma za mikopo ya kawaida na inayozingatia misingi ya shariah kupitia kitengo chake cha imaan finance.

Kwa kuzingatia nafasi yake kubwa sokoni na kuendelea kujijengea sifa kama mshirika wa kuaminika katika uwekezaji, itrust inalenga kutumia programu hii kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya fedha nchini huku ikiunga mkono ukuaji wa uchumi shirikishi.

Hivyo awekezaji wanaweza kupata taarifa zaidi na kuwasilisha maombi ya kuwekeza katika hatifungani hiyo kupitia majukwaa ya kidijitali ya itrust ikiwemo aplikesheni, tovuti na mfumo wa mtandaoni wa kampuni hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana (CMSA) CPA. Nicodemus Mkama , Alfred Mkombo – Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango (CMSA) alisema Utoaji wa hatifungani hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha yaani Financial Sector Development Master Plan 2020/21 na 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

“Hatifungani hii inawezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo yaani Tanzania Development Vision 2050 (DIRA 2050) yenye lengo la kuwa na uchumi shindani, himilivu na jumuishi kwa maendeleo endelevu kwa watanzania wote, ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya ujasiriamali,

Masoko ya Mitaji nchini ni imara, himilivu na yanaendelea kushamiri huku mamlaka ya Masoko ya Mitaji na dhamana (CMSA) itaendelea kutekeleza mikakati yenye lengo la kuchagiza na kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.

Aidha makampuni na taasisi katika sekta binafsi na umma zinatakiwa kutumia fursa katika masoko ya mitaji kupata fedha za kutekeleza shughuli za kukuza na kuendeleza biashara na miradi ya maendeleo.

“kampuni zenye leseni ya kutoa huduma katika masoko ya mitaji zinatakiwa kuendeleza mikakati ya kuanzisha bidhaa bunifu zinazopanua na kuongeza fursa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa,anasema

Katika hatua nyingine Afisa mwandamizi kitengo cha utafiti Samai Shirima alieleza hatifungani ya i trust bond ina ukomavu wa miaka minne na kila mwaka mtu atapokea asilimia 13 ambayo itagawanywa katika malipo ya awamu nne.

mwekezaji atakuwa na uhakika wa kupata fedha kila tarehe 29 ya mwezi Machi, Mwezi Juni,Septemba na Desemba,anasema

Vijana wengi na ambao hata hawana uwezo mkubwa wakiuchumi wanaweza kuwekeza na i Trust Bond.

i Trust tumekuja na njia ya kidigitali na unaweza kufungua akaunti kupitia simu yako ya mkononi (Smartphone) yako ukiwa popote ulipo kupitia application ya i Trust unaytoweza kuipakua kupitia play store au App store,anasema