November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Harambee ujenzi wa kanisa la TAG yaingiza Mil. 91

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

VIONGOZI mbalimbali wa chama na serikali wameungana na waumini wa kanisa la TAG Maranatha Miracle Centre Mjini hapa katika ibada maalumu ya kuchangia ujenzi wa jengo la kanisa hilo litakalokuwa na uwezo wa kuchukua waumini 2000.

Katika harambee hiyo iliyoongozwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa Tabora, Ramadhan Kapela kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Lameck Nchemba, jumla ya sh mil 91 zimechangwa ili kufanikisha ujenzi huo.

Akiongea katika ibada hiyo Mstahiki Meya amesema kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa Madhehebu ya dini katika maendeleo na kudumishwa amani na utulivu wa nchi.

Amemwomba Mchungaji Kiongozi na waumini wa kanisa hilo kuendelea kuliombea taifa na kumwombea Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ili mipango ya maendeleo anayopanga kwa ajili ya wananchi ifanikiwe kwa asilimia zote pasipo kikwazo chochote.

Mstahiki Meya amebainisha kuwa ujio wake katika ibada hiyo unatokana na mahusiano mazuri baina ya serikali na Viongozi wa dini, hivyo akaomba waendelee kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu pasipo kuvunja sheria.

‘Mheshimiwa Waziri anawasalimu sana na yupo pamoja nanyi, amenituma niwaletee salamu na ameahidi kuwachangia kiasi cha sh mil 10 ila kwa kuwa ana marafiki wengi amesema ataomba wamuunge mkono ili zifike sh mil 35’, amesema.

Ameongeza kuwa kwa niaba ya halmashauri ya manispaa hiyo watatoa kiasi cha sh mil 2 ili kufanikisha ujenzi huo, wengine walioahidi ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora Deusdedith Katwale sh mi 3 na Mkuu wa Mkoa huo Paul Matiko Chacha ambaye atakabidhi mchango wake wakati wowote.

Viongozi wengine walioahidi kuchangia ujenzi huo ni familia ya Mchungaji Lutengano sh mil 3.5, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora laki 5, Mwakilishi wa Askofu wa Kanisa la KKKT laki 1na Mwendesha Mashtaka wa Serikali Mkoani hapa laki 5.

Wengine ni Askofu John Mkurugenzi wa shule ya Eternal Life laki 5, Luteni Kanali Jimmy wa Jeshi la Wananchi Brigedi ya Tabora laki 6 na Mwangalizi wa Makanisa ya TAG Section ya Cheyo laki 5 na mifuko 10 ya saruji.

Wengine ni Kada wa CCM na Mwandishi wa Habari wa Magazeti ya Chama sh laki 5, Mwakilishi wa CHADEMA laki 2, Mkurugenzi Hospitali ya Hosiana sh mil 2, waumini wote wa kanisa hilo na wadau wengine wengi.