January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hamburg, Dar kujadili mabadiliko ya tabianchi

Na Irene Clemence,timesmajira,Online

MIONGONI mwa shughuli zitakazofanyika katika  Maadhimisho ya miaka 12 ya urafiki wa miji kati ya Jiji la Dar es Salaam na Hamburg,wageni zaidi ya 30 wanatarajia kuja nchini na kuja kujadili mambo mbalimbali ikiwemo changamoto na fursa zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya wananchi wa majiji hayo.

Akizungumza hayo leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti  Kamati ya Maandalizi  ya maadhimisho ya miaka 12 ya urafiki wa miji kati ya Jiji la Dar es Salaam  na Jiji la Hamburg,Dkt.Sylvia Ruambo alisema wadau hao kutoka katika pande hizo mbili wanatoka katika taasisi mbalimbali za serikali, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Amesema  kupitia fursa hii wameona kuna umuhimu wa wao kukutana na kufanya majadiliano hayo ikiwa ni sehemu za juhudi za kushirikiana na serikali katika jitihada zake za jukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

“Urafiki kati ya majiji hayo umechangia na kusaidia  kuboresha huduma katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na sekta ya afya, mazingira, elimu, utafiti na utamaduni,amesema na kuongeza

“Aidha majiji hayo yamewasaidia wataalamu wake na  wananchi kufanya ziara za kujifunza, kubadilishana uzoefu katika utendaji wa kazi na utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,”amesema Dkt.Ruambo

Amesema katika kipindi cha miaka 12 ya urafiki huo wa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Chuo kikuu cha Ardhi na Jiji la Humburg wamekuwa mstari wa mbele katika uandaaji wa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kufanya utafiti kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kukabiliana nazo kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mazingira.

Amesema urafiki wa jiji la Dar es Salaam na jiji la Humburg ulianza rasmi  Julai 2010 baada ya majiji hayo kutia saini hati ya makubaliano ya kuanzishwa kwa urafiki huo hivyo maadhimisho ya miaka 12 ya urafiki wa majiji unatarajiwa kuwakutanisha wadau wengi kutoka katika sekta mbalimbali ambao watashauriana pia kuhusu njia bora ya kuimarisha urafiki huo na kuongeza idadi ya watu wanaonufaika na fursa zitokanazo na uhusiano huo.