January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri zatakiwa kupima afya ya udongo ili kuwasaidia wakulima

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI za wilaya nchini kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) wametakiwa kutembelea wakulima vijijini na kuwasaidia kupima afya ya udongo ili kutambua aina ya mazao yanayofaa kulimwa katika maeneo yao.

Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde alipokuwa akihitimisha maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika uwanja wa Chipukizi Mjini Tabora.

Amebainisha kuwa huduma hiyo inatolewa bure hivyo mkulima asidaiwe gharama yoyote lengo likiwa kumsaidia kufanya kilimo chenye tija ili kuongeza uzalishaji na kujikwamua kiuchumi.

Silinde ameahidi kuwa serikali ya awamu ya sita itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya wakulima ili kuwasaidia kufanya kilimo chenye tija kitakachowanufaisha zaidi.

Amepongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ilani nzuri ya maendeo ambayo imeendelea kutekelezwa na serikali yake kwa vitendo.

Kuelekea msimu mpya wa kilimo Naibu Waziri ameelekeza wakulima wote kuhakikisha wamesajiliwa kwenye mfumo ili kunufaika na mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali.

Amewataka waliosajiliwa kwenda kuhakiki taarifa zao na ambao bado wakajiandikishe kwa Watendaji wa Mitaa na Vijiji ili waingizwe katika mfumo.

Aidha ameagiza Mamlaka ya Udhibiti Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha mbolea ya ruzuku inayotolewa na serikali inawafikia wakulima kwa wakati na karibu na maeneo yao.

Pia ameagiza kuchukuliwa hatua stahiki wale wote watakaobainika kukwamisha zoezi la usambazaji mbolea hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent amemweleza Naibu Waziri kuwa wameboresha mfumo wa usambazaji mbolea na wataendelea kuwapa elimu wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea hiyo.

Amebainisha kuwa katika maadhimisho hayo jumla ya wakulima 278 wamepatiwa Elimu na zaidi ya wananchi 6000 wamehudhuria maonesho hayo na kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo bora.