November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora, Dkt.John Pima.

Halmashauri yapata dawa ya uhaba vyumba vya madarasa

Na Allan Ntana,TimesMajira Online

SERIKALI ya Awamu ya Tano imefanya kazi kubwa sana ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari hapa nchini, lakini licha ya juhudi hizo changamoto kubwa iliyopo sasa ni uhaba wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, matundu ya vyoo na madawati.

Katika kukabiliana na tatizo hilo serikali imeelekeza halmashauri zote kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ili kufanikisha utekelezaji miradi yao ikiwemo kumaliza tatizo la uhaba wa vyumba vya madarasa, vyumba za walimu na matundu ya vyoo.

Aidha, mbali na fedha za ruzuku zinazotolewa na serikali kuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo, serikali imesisitiza sana ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ikiwemo kuhamasisha wananchi au wadau kuchangia miradi ya maendeleo.

Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji, Dkt.John Pima imekuja na mkakati shirikishi wa elimu ya kujitegemea ambao unatekelezwa kwa vitendo shuleni na katika jamii.

Dkt.Pima anazungumza na gazeti hili na kubainisha kuwa elimu ya kujitegemea inalenga kumpa stadi za maisha mtoto wa shule kwa kumjengea uwezo, ujuzi, mbinu za kutumia mazingira na rasilimali zilizopo kutatua shida iliyopo.

Ufafanuzi wa dhana ya kujitegemea

Dkt.Pima anafafanua kuwa, elimu hii ni muhimu sana kwani utafiti unaonesha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba au kidato cha nne na kukosa nafasi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu wengi wao hupoteza mwelekeo, hivyo kuanza kuzurura ovyo mitaani au kujiingiza katika vitendo visivyofaa ikiwemo wizi.

Anaeleza kuwa dhana ya elimu ya kujitegemea iliasisiwa na hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1967 akiwa na lengo la kumpa ujuzi na mbinu bora Mtanzania ambapo mwaka 1973 elimu ya kujitegemea iliingizwa kwenye mfumo rasmi na kuanza kufundishwa shuleni, kabla ya kufifishwa.

Anasisitiza kuwa, lengo la elimu hiyo shuleni sio tu mwanafunzi kushiriki kufyatua matofali, kulima bustani au kufanya kazi za mikono bali kuandaa ubongo na fikra zake ili aweze kujitegemea kutatua shida zake hata baada ya kumaliza shule.

Aidha anaongeza kuwa, elimu ya kujitegemea inamjengea mwanafunzi utayari wa kufanya kazi kwa kujitolea, kudumisha ushirikiano, mbinu za ujasiri, ukakamavu na kutengeneza taifa la vijana hodari, wazalendo na wachapa kazi.

Wanafunzi wamepata manufaa gani

Dkt.Pima anashuhudia kuwa, elimu ya kujitegemea kwa vitendo ambayo wameanza kuitekeleza mwaka jana katika shule zote za msingi na sekondari imekuwa mwarobaini wa uhaba wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na vyoo.

Anabainisha kuwa. elimu hii imekuwa msaada mkubwa sana kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo kwani wanafunzi wamehamasika kujifunza stadi za maisha kwa vitendo kupitia ufyatuaji tofali, kupanda miti na kilimo.

Matokea makubwa yaliyopatikana

Dkt.Pima anaeleza kuwa, baada ya dhana hiyo kuwasilishwa kwa wadau wa elimu zikiwemo kamati za maendeleleo ya kata, bodi za shule, wakuu wa shule na watumishi na kuafikiwa sasa matunda yameanza kuonekana.

Anabainisha kuwa, kupitia dhana hiyo shule zimeweza kufyatua jumla ya matofari 2,573,429 ya udongo na kuchomwa ambapo matofali 1,962, 213 yalifyatuliwa katika shule za msingi na 611, 216 katika shule za sekondari.

Anabainisha kuwa matofali hayo yamejenga vyumba 93vya madarasa kwa shule za msingi, vyumba 56 kwa shule za sekondari, nyumba 11 za walimu wa elimu ya msingi, matundu 69 ya vyoo vya shule za msingi na 36 kwa shule za sekondari.

Mafanikio katika kilimo

Dkt.Pima anabainisha kuwa kupitia elimu hiyo kila shule imeweza kupanda miti ya kivuli na matunda na kulima mazao mbalimbali ikiwemo korosho, mahindi, alizeti, viazi, karanga na mpunga, hivyo kuanzia mwakani watakula chakula shuleni.

Anafafanua kuwa, elimu ya kujitegemea imewezesha wanafunzi wa shule za msingi kulima jumla ya ekari 421 za mashamba ya mazao mbalimbali yakiwemo korosho ekari 118, mahindi (143), alizeti (16), viazi (41), karanga (80) na mpunga ( 23).

Aidha, anaeleza kuwa kwa upande wa shule za sekondari wamefanikiwa kuanzisha mashamba ya mazao mbalimbali yenye ukubwa wa ekari 121ambayo ni korosho ekari 15, miti ya mbao ( 71.8), matunda (5), miti ya kivuli (2,467).

Manufaa kwa halmashauri

Anafafanua kuwa, mpango huo umeisaidia halmashauri kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za matengenezo ya miundombinu hiyo katika shule zote ambapo imetumia kiasi cha sh.milioni 416.3 tu za mapato yake kumalizia miradi hiyo yote.

Mikakati ya halmashauri

Anabainisha kuwa, kwa mwaka 2020/2021 wanatarajia kuboresha kilimo hicho katika shule zote ili walime mazao ya chakula na biashara na mavuno yatakayopatikana yatatumika kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi.

Anaongeza mkakati mwingine kuwa ni kila shule ya sekondari kufyatua matofali 1,658,934 na kushirikisha jamii katika ujenzi wa miundombinu yote inayohitajika mashuleni ikiwemo madarasa, maabara, mabweni, maktaba na matundu ya vyoo.

Madiwani wanena

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Silambo, Ibrahim Isaya Kifoka anaeleza kuwa, mfumo huo umeifanya halmashauri hiyo kuwa mfano wa kuigwa na halmashauri zingine za mkoa huo.

Diwani wa Viti Maalum Kata ya Uyowa, Batseba Daniel Bastola (CCM) anabainisha kuwa mfumo huo umesaidia kuleta maendeleo ya moja kwa moja kwa wananchi hivyo utasaidia sana kutengeneza vijana wa taifa la kesho walio jasiri.

Afisa Elimu Sekondari anena

Afisa Elimu Sekondari wa halmashauri hiyo, Jimmy Nkwamu anapongeza wakuu wa shule za msingi na sekondari kwa jinsi wanavyoshirikisha wanafunzi na jamii kwa ujumla katika kufanikisha elimu ya kujitegemea.

Anaongeza kuwa, elimu hiyo ina umuhimu mkubwa sana katika makuzi na malezi ya wanafunzi shuleni ambapo hujifunza mbinu bora za kilimo cha kisasa, ufugaji, uanzishaji na utunzaji bustani za maua, mboga mboga, miti na matunda.

Ushauri

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Haruna Kasele anashauri mfumo wa elimu ya kujitegemea urejeshwe katika shule zote ili kujenga jamii ya watu wenye uzalendo wa kweli na iliyo tayari kujitolea katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Anashauri serikali itumie mafanikio ya halmashauri Kaliua kuhuisha na kuhaisha mfumo huo nchini kwa lengo la kutengeneza jamii yenye kuishi katika misingi bora yenye kuliletea taifa maendeleo makubwa.

Naye Mkurugenzi Dkt.Pima anashauri serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia Sheria ya Elimu ya 1978 na marekebisho yake, sera ya elimu na utamaduni ya 1995 na 2014 kutumia mfumo huu ili kujenga kizazi kipya cha wachapa kazi na kupunguza utegemezi kwa serikali kuu hususani katika suala la chakula mashuleni.