September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Kaliua yaweka mikakati kuongeza uzalishaji chakula

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua Mkoani hapa imeanzisha mkakati wa kuwa na mashamba darasa ya mfano katika shule zote za msingi na sekondari katika kila kata ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Jerry Daimon Mwaga alipokuwa akiongea na Mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake juzi ambapo alibainisha kuwa wamedhamiria kumaliza kilio cha uhaba wa chakula.

Alisema utekelezaji programu hiyo tayari umeanza, wataanza kuzalisha zao la mahindi katika shule hizo na kwa kuanzia wamenunua kilo 2,000 sawa na tani 2       za mbegu bora ya mahindi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tumbi (TARI).

Alibainisha kuwa mbegu hizo zimesambazwa katika shule za msingi na sekondari na kwa Maofisa Kilimo wa Kata ambao wamepewa dhamana ya kusimamia mpango huo ili kuhakikisha unapata mafanikio makubwa katika maeneo yao.

Mwaga aliongeza kuwa mkakati huo utahusisha uanzishwaji wa mashamba ya mfano ya mazao chakula na biashara ili kupanua wigo wa upatikanaji chakula cha kutosha na kuingiza mapato kupitia mazao hayo.

Alifafanua kuwa halmashauri kwa kushirikiana na Taasisi ya TARI Tumbi na Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu (TOSCI) tayari wamefanya ukaguzi wa mashamba ya kuzalisha mbegu bora za muhogo na wakulima 12 wa mfano wamepewa elimu.

Wakulima hao kutoka kata za Ugunga, Ukumbisiganga, Zugimlole, Igagala na Usenye tayari wamekidhi vigezo na mbegu ambazo zimeanza kuzalishwa zinafaa kusambazwa kwa wakulima wengine.

Akieleza malengo ya mpango huo, alisema utasaidia Wilaya hiyo kuwa na chakula cha kutosha na huduma ya chakula kutolewa katika shule zote za msingi na sekondari ili kuchochea wanafunzi kusoma kwa bidii na kuongeza ufaulu wao.

Mkurugenzi alibainisha kuwa hadi sasa jumla ya ekari 555 za mazao ya chakula na ekari 18 za mazao ya biashara zimelimwa katika shule 132 na kupandwa mbegu za kisasa zilizotolewa na halmashauri.

Aidha katika kuhakikisha wakulimwa wanaolima zao la tumbaku wilayani humo nao wanapata manufaa makubwa, alisema wamewawezesha jumla ya mifuko 98,353 ya N.P.K, mifuko 25,633 ya CAN na mifuko 22,942 ya UREA ikiwemo mbolea ya ruzuku tani 779.4 za UREA.

Mwaga alipongeza Wataalamu na Watendaji wake katika halmashauri hiyo kwa ushirikiano wao mkubwa ambao umewezesha halmashauri hiyo kuendelea kuongoza katika suala zima la ukusanyaji mapato katika Mkoa mzima ikiwemo ufuatiliaji mikopo ya wajasiriamali ambapo katika miezi 3 tu sh mil 43.4 zimerejeshwa.

Mkurugenziwa Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora Jerry Daimon Mwaga akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo katika moja ya vikao vya halmashauri hiyo, katikati ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Jafael Lufungija na Mbunge wa Jimbo la Ulyankulu lililopo wilayani humo Rehema Migira. Picha na Allan Vicent