January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Halmashauri Ilemela kuanza kutekeleza miradi ya elimu

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza

KATIKA kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya elimu,Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Aprili mwaka huu, imepokea kiasi cha milioni 399.2 kutoka Serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary,wakati akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika katika halmashauri hiyo.

Mhandisi Apolinary,amesema katika ya fedha hizo kiasi cha milioni 80,walipeleka shule ya sekondari Sangabuye kwa ajili ya ujenzi wa bweni huku shule za sekondari, Bujingwa, Nyamanoro na Kangaye kila moja walipatiwa milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kwa kila shule.

Amesema pia shule za sekondari Nyamanoro na Kirumba kila moja walizipa milioni 13.2,kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 12 kwa kila shule.

Aidha amesema,kwa upande wa elimu msingi,shule zilizonufaika na fedha hizo Ni pamoja na Igogwe,Kaselya na Buswelu ambazo kila moja zilipokea milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kila shule.

Huku shule za msingi Kaselya,Buswelu, Hekima na Tumaini kila moja zilipatiwa milioni 13.2,kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 12 kwa kila shule.

Sanjari na hayo,Mhandisi Apolinary, amesema katika halmashauri hiyo wana uhaba wa zaidi ya vyumba vya madarasa 2,000 shule za msingi na sekondari zaidi ya madarasa 300.

Huku uhaba wa madawati pia upo na ametembelea shule nyingi na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto kwani wahitaji ni wengi.

Hivyo aliwaomba madiwani kufanya harambee pia katika maeneo yao kuwepo na karakana ya kutengeneza madawati ambapo watanunua miti na kutengeneza wenyewe maana kwa kununua hawata weza maana uhitaji ni mkubwa.

Wakichangia taarifa hiyo,baadhi Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,wamemuomba Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuja na mpango mkakati wa kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya elimu ndani ya halmashauri hiyo.

Diwani wa Kata ya Shibula Swila Dede, amemuomba Mkurugenzi azungukie halmashauri yake kwani kuna maboma ya madarasa hayajakamilika pia nyumba
nyumba za walimu zimejengwa hazijakamilika.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary,wakati akiwasilisha taarifa yake katika kikao cha Baraza la Madiwani kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2020/2021 kilichofanyika katika halmashauri hiyo.Picha na Judith Ferdinand

“Walimu wanaishi kwa shida na nyumba zipo hazijakamilika na kuna madarasa pia hayajakamilika,niombe ukapitie halmashauri yako ili uje na mpango kabambe,kamati zako za fedha zipitishe kazi ziendelee za kumalizia nyumba na madarasa ambayo yakimalizika utosikia kelele,”amesema Swilla.

Diwani wa Kata ya Kitangiri,Donald Ndaro amesema katika shule ya msingi Kitangiri C kuna uhaba wa madawati ambapo darasa la sita kuna wanafunzi wengi na madawati yapo machache.

Hivyo ameomba kwa kusema kuwa kama kuna uwezekano changamoto hiyo itatuliwe ili watoto waweze kusoma katika mazingira mazuri.

Naye Diwani wa Kata ya Nyamanoro, George Maganiko,amesema katika shule ya msingi Mwenge iliopo katika kata yake kuna tatizo la uhaba wa madawati pamoja na madarasa licha ya kuwa wananchi walitoa nguvu zao kujenga maboma Ila mpaka sasa hayajamaliziwa.

Maganiko ameiomba halmashauri hiyo iwasaidie katika umaliziaji wa madarasa katika shule za kata yake ambayo hayakukamilika kwa wakati.