Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Chunya
UONGOZI wa Halmashauri ya wilaya Chunya mkoani Mbeya umesema kuwa hautakuwa tayari kuona uzembe utakaojitokeza katika ujenzi wa stendi mpya ya mabasi inayotarajiwa kuanza kujengwa katika kijiji cha Sinjilili kata ya Itewe wilayani humo.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 9,2024 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbugani, Bosco Mwanginde wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa stendi hiyo na MALK CONSULTANTS LTD ambaye ndiye msanifu wa mradi huo.
“Katika wilaya hii ya Chunya Sitakuwa tayari kwa uzembe wowote ambao utajitokeza au kuonekana kwa misingi hiyo mkataba uliosaniwa leo ili mkandarasi aweze kuanza kazi ambao ulikuwa unasubiriwa kwa muda mrefu hivyo mimi na baraza langu la madiwani tutasimamia kwa weledi mkubwa na kwa muda uliowekwa kwani fedha ipo tunatumia mapato ya ndani kwa kushirikiana na taasisi za kifedha hivyo tuna uhakika wa asilimia 100 na mradi huu utakamilika na wananchi watanufaika”amesema Mwanginde.
Aidha Mwanginde amesema kwa kushirikiana na madiwani,Mkuu wa Wilaya wapo tayari kupokea maelekezo kutoka kwa mkuu wa mkoa kwa ushauri kwa ajili ya miradi inayoendelea katika wilaya hiyo ikiwemo mradi wa stendi uliosaniwa .
Akitoa taarifa ya ujenzi wa stendi hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Chunya,Tamimu Kambona amesema kuwa wazo la ujenzi wa stendi mpya lilitokana na uhitaji mkubwa wa huduma ya stendi baada kutokana na ongozeko kubwa la idadi ya abiria na mabasi makubwa na madogo lilopelekea utoaji wa huduma zamsingi kwa abiria wa eneo la kupaki magari stendi ya kisasa kutotosheleza.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa ujenzi wa stendi hiyo utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 9 kuanzia Septemba 16,2024 hadi Juni 15,2025 na kwamba baada ya kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na kipindi cha mradi cgha miezi 12 kwa mkandarasi na mshauri elekezi ili kufanya marekebisho kwa maeneo ambayo yatakuwa yana changamoto kiufundi.
Kambona amesema lengo la mradi huo ni kutoa huduma bora ya usafirishaji katika wilaya ili kutatua kero zilizopo katika stendi ya sasa lakini ni pamoja na kutekeleza agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara ya kikazi wilayani humo mwezi Agosti ,2022 kuwa ujenzi wa stendi utekelezwe kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri ili kutatua kero za wananchi .
Akielezea zaidi Tamimu amesema kuwa lengo linguine ni kuongeza wigo es vyanzo vya kudumu vya kukusanya mapato ili kuongeza tija katika wilaya ya chunya na Taifa kwa ujumla baada ysa kukamilisha marejesho ya mkopo.
Hata hivyo Kambona amesema gharama za mradi huo zinatarajiwa kutumia zaidi ya Bil.3 ambapo gharama hizo zinajumuisha pamoja kumlipa Mhandisi mshauri elekezi na mkandarasi na fedha hizo zitatoka mapato ya ndani ya halmashauri na mkopo toka benki.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Juma Homera, amemtaka mkandarasi kufanya kazi hiyo kwa ubora, wakati na uadilifu.
“Nitoe wito kwa taasisi zote TANESCO, watu wa Maji na wengine hakikisheni huduma hazikosekani hapa ili mkandarasi afanye kazi na stendi hii ikamilike kwa wakati. Chunya tunaenda vizuri madude yanaendelea kujengwa jengo la Halmashauri limejengwa, hapa tunashusha dude lingine (Stendi mpya Chunya) na madude mengine huko yanaendelea yote haya ni kwasababu Chunya mlichagua vizuri na msije mkachagua viongozi wa hovyo, viongozi wa hovyo si mnawafahamu!”amesema Homera.
Pia,Homera ameitaka Serikali ya wilaya ya Chunya kuendelea kuwa karibu na mkandarasi na kusimamia ujenzi huo ili ukamilike kwa wakati na kuleta manufaa kwa wasafiri na wananchi kwa ujumla pamoja na Serikali kwa ujumla.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi