Na Jackline Martin, TimesMajira Online
WANAWAKE wanaokabiliwa na changamoto ya kupata watoto jijini Dar es Salaam wameanza kupata suluhisho baada ya kituo cha uzazi cha Chennai Fertility Center (CFC) kuanza kuwapatia huduma ya ushauri bure kwa siku tatu kuanzia jana.
Kituo hicho kinajivunia kwa kuvunja rekodi ya kutoa huduma ya uzazi kwa mafanikio kwa zaidi ya wanawake 50,000 kote ulimwenguni na kutambulika mara kwa mara kama kliniki bora zaidi ya uzazi kupitia huduma yao ya upandikizaji wa mimba (IVF).
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya Matibabu na Afya (24th mediexpo Afrika), Mwenyekiti na Mkurugenzi wa CFC, Dkt. Thomas alisema huduma ya ushauri wa hatua kwa hatua kwa mama mwenye changamoto ya uzazi inatolewa bure katika maonesho hayo ambayo yatamalizika Februari 18, mwaka huu.
“Katika maonyesho haya kuna madaktari wawili ambao wametoka Chennai na wapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa yule mama aliyekusa mtoto na elimu hii ni bure” alisema.
Dkt. Thomas alisema Kituo cha CFC kina vifaa vya maabara vya kati kwa wataalam wote wa IVF ambao wanataka kuwatibu wagonjwa wao katika mazingira ya hali ya juu.
Alisema kituo kinawapa wataalam udhibiti kamili juu ya taratibu za wagonjwa wao.
Kwa upande wake, Mratibu wa kituo cha CFC, Shose Komba aliwataka wakina mama ambao walikata tamaa ya kupata watoto kufika katika banda lao ili kukutana na madaktari bingwa ambao wanatoa ushauri wa uzazi .
“Wale wote mliokata tamaa ya kupata watoto madaktari wapo hapa na wanatoa huduma hii bila malipo, daktari anakuja anakupa maelekezo ya nini unahitaji ili kama kuna vipimo au dawa utaandikiwa na kwenda kuanza kutumia,” alisema.
Naye mmoja wa washiriki aliyehudhuria maonyesho hayo Sifa Samson amesema kuwa fursa ya upandikizaji mimba kwa wanawake itasaidia sana hususa ni katika kupunguza gharama za matibabu kwa watanzania wanaosafiri kupata matibabu hayo nje ya nchi huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye maonyesho hayo ili kupata huduma hiyo
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa