January 18, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gwajima azindua madarasa mawili

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kabla ya kuhudhurisha mahafali ya 5 ya Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kisangara Waziri Dkt. Gwajima alizindua rasmi madarasa mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 370 na ofisi mbili yaliyojengwa kwa fedha za ndani kwa kutumia wataalamu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii na Ufundi Mabughai.

Aidha, ameweka pia jiwe la msingi katika ujenzi wa bweni la wanafunzi litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 104 na kuipongeza Taasisi ya Ustawi wa Jamii kwa juhudi za ujenzi wa miundombinu katika kampasi hiyo zinazoendelea na utunzaji wa mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Lulu Mahai ametoa wito kwa wadau wa malezi na makuzi kutumia Taasisi ya Ustawi wa Jamii kupata taaluma hiyo, huku akieleza kuwa Mipango ya muda mfupi ujao ni Kujenga Maktaba ya wanafunzi itakayo kuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 na Kuanza kudahili wanafunzi wa Shahada ya Ustawi wa Jamii katika kampasi ya Kisangara.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Abdallah Mwaipaya ambaye aliambatana na Mh. Waziri Gwajima katika mahafali hayo amesema Taasisi ya Ustawi wa Jamii Kisangara imekuwa na manufaa kwa wilaya hiyo kutokana na kuendelea kupanuka kitaaluma hivyo ni msaada mkubwa kwenye jamii baada ya wahitimu hao kuwa tayari kuhudumia jamii, akiwafananisha na askari Miamvuli wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum watakao msaidia Mh. Waziri Gwajima kustawisha Tanzania.