December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Gombe hifadhi yenye maajabu ya sokwe mtu

Na Mwajabu Kigaza

HIFADHI ya Gombe ni kati ya hifadhi 16 miongoni mwa hifadhi muhimu nchini Tanzania yenye vivutio mbalimbali vinavyosababisha watalii kutoka nje ya nchi na wale wa ndani kupendelea kufika katika hifadhi hiyo kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo.

Awali Hifadhi ya Gombe ilikuwa ni Game Reserve ambapo ilitumiwa na wakazi wa vijiji jirani kufanya shughuli zao za uzalishaji mali ikiwemo kupata kuni kwa ajili ya nishati ya kupikia.

Sambamba na kupata mbao kwa ajili ya kuuza, lakini pia ukataji wa misitu kwa ajili ya kupata mkaa, shughuli za uvuvi wa mazao ya samaki na dagaa pamoja na uwindaji wa wanyama.

Mwaka 1968 Serikali iliamua kulifanya eneo hilo kuwa Hifadhi ya Taifa Gombe ambayo ni hifadhi ya pili kwa udogo kuliko zote nchini ikiwa na kilomita za mraba 56 tu, lakini ina umaarufu mkubwa unaotokana na kivutio kikubwa cha sokwe mtu ambaye kwa asilimia 98, maisha yake yanafanana sana na maisha ya binadamu.

Hifadhi hiyo ilipata umaarufu mkubwa mara baada ya kufanyika kwa tafiti ya baadhi ya wanyama ambapo sokwe alionekana kuwa wa kipekee zaidi.

Mtafiti wa tabia ya sokwe duniani, Jane Goodall alifanya utafiti juu ya maisha na tabia za sokwe kwa miaka 40 na kuandika vitabu kadhaa kuhusu viumbe hao.

Jamii ya sokwe ya Kasakela, ipo katika vitabu na hati kadhaa na hatua hiyo ilichochea umaarufu mkubwa wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe.

Wanyama wengine wanaopatikana katika hifadhi hii ni pamoja na nyani wenye mkia mwekundu na wa bluu, pongo, ngurue pori na Hifadhi ya Gombe haina wanyama wakali kama simba na chui na hivyo kutoa fursa kwa watalii kufanya utalii wao kwa miguu kutokana na usalama uliopo katika hifadhi hiyo.

Usafiri mkubwa wa kuelekea katika Hifadhi ya Gombe ni usafiri wa maji kwa kutumia boti na ni kilomita 16 kutokea Kigoma Mjini, katika jitihada za kuboresha huduma ya usafiri Gombe iliandaa boti kulingana na uwezo wa kila mtu ikiwemo ya mwendo kasi dakika 25.

Boti za mwendo wa kawaida ambazo hutumia saa moja na nusu, lakini pia wale wanaohitaji usafiri wa pamoja na wananchi pia wanapata fursa hiyo.

Mafanikio

Baadhi ya mafanikio yaliyojitokeza ni mara baada ya idara ya utalii ilipoanza ikiwa na jukumu kubwa la kuhakikisha utalii katika Hifadhi ya Gombe unakuwa na kuongeza watalii wa nje na ndani ambapo kwa muda mfupi hifadhi hiyo imekuwa na mafanikio makubwa katika suala zima la kuongeza watalii kutokana na vivutio vilivyopo.

Happiness Kiemi ni mhifadhi utalii ambaye anaeleza baadhi ya mafanikio ni pamoja na kuibua vivutio vingi ambavyo vimekuwa kichocheo kikubwa cha kuongeza utalii katika hifadhi hiyo.

Anasema, mbali na wanyama, lakini pia jitihada zilifanyika za kuhakikisha shughuli za kibinadamu katika eneo la hifadhi zinaondolewa ili kutunza mazingira.

Utunzaji wa mazingira ulisababisha kuwepo kwa mapori na msitu mzuri unaofaa kufanyika kwa shughuli za utalii kutokana na kuwepo kwa mandhari nzuri, lakini pia wanyama kupata maeneo ya utulivu.

Kivutio kingine ni maporomoko ya maji yaliyopo ndani ya hifadhi, ndege, mazao ya samaki na dagaa wa aina mbalimbali ambao wanahifadhiwa ndani ya hifadhi, lakini pia ni pamoja na utalii wa kihistoria ambao umekuwa kivutio kikubwa kwa wageni wanaofika katika hifadhi hiyo kujua historia ya sokwe na maisha yao kwa ujumla.

Lakini pia jamii kuendelea kupatiwa elimu ya ulinzi shirikishi kuhakikisha maeneo yaliyohifadhiwa yanaendelea kuwa endelevu kwa sasa na baadae, lakini pia kushirikiana katika uhifadhi wa wanyama pamoja na kulinda rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi.

Kuanzishwa kwa vikundi shirikishi katika vijiji vilivyopo ambapo kuna vijiji vitano vilivyopo karibu na hifadhi na vikundi hivyo vimekuwa vikitumika kutoa elimu kwa jamii umuhimu wa kulinda na kutunza hifadhi kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Vikundi hivyo pia vimekuwa vikinufaika kupitia watalii wanaofika katika Hifadhi ya Gombe na hiyo pia ikiwa ni moja ya ubunifu, ambapo vikundi hivyo hutoa burudani ya ngoma za asili, lakini pia hutengeneza vitu vya asili hii yote ikiwa ni njia za kuongeza utalii katika hifadhi hiyo.

Lakini pia kupunguza matukio ya ujangili ambapo awali kulikuwa na shughuli za kijamii zilizokuwa zikiendelea na kupitia vikundi hivyo imekuwa chachu ya kuondokana na uvamizi katika hifadhi licha ya kuwa na ongezeko kubwa la wananchi.

Sambamba na kuwapatia wananchi miti waweze kupanda kwenye maeneo yao ili tu kuhakikisha jamii inayozunguka hifadhi haitumii rasilimali zilizopo katika hifadhi na hilo linatokana na utunzaji wa misitu yao wenyewe, lakini pia elimu wanayopatiwa ya kulinda hiyo misitu kwa manufaa yao.

Kutoa elimu katika maeneo ya shule, vyuo na ofisini kuona umuhimu wa kutembelea hifadhi ambapo hii imeongeza pia watalii wa ndani japo kwa kiwango kidogo, pia ni kutumia mitandao ya kijamii kutoa elimu, vipeperushi, mabango na vyombo vya habari sanjari na kutoa elimu kwa watumishi namna ya kuwapokea wageni.

Pia kuongezeka kwa watalii ambapo hadi sasa watalii wamefikia 2,000 ambao wanafika katika hifadhi na watilii wengi wakiwa ni wale wa kutoka nje ya nchi huku wazawa wakiwa ni kwa kiwango cha chini.

Changamoto

Palipo na mafanikio hapakosi changamoto ambapo Happiness anaeleza baadhi ya changamoto ambazo ni kikwazo cha kufikia malengo ya kukuza utalii katika hifadhi hiyo kuwa ni pamoja na miundombinu mibovu ya usafiri na kusababisha kukosa watalii wa kutosha licha ya kuwepo kwa uhamasishaji mkubwa katika jamii.

Kwa upande wa miundombinu barabara imekuwa ni changamoto kubwa kwa wageni ikiwa usafiri mkubwa ni wa maji ambapo mara kadhaa kumekuwa na kadhia ya kuchafuka kwa Ziwa Tanganyika.

Hivyo kusababisha kuahirishwa kwa safari ama kuwepo kwa ucheleweshwaji wa safari jambo linalochangia watalii wengi kukata tamaa.

“Kuna wakati hali ya hewa katika Ziwa Tanganyika inakuwa mbaya na hii inatokana na kuwepo kwa upepo pamoja na mawimbi kushamiri na hivyo wageni wengi hukata tamaa ya kutumia vyombo vya usafiri kwa kuhofia usalama wa maisha yao,”anasema Happiness.

Akisisitiza changamoto ya usafiri Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Gombe, Donatus Bayona anasema, kukosekana kwa usafiri wa barabara imekuwa ngumu kwa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika hifadhini na hii inachangiwa na gharama kubwa za usafirishaji wa kutumia boti ambayo inatumia gharama kubwa ya mafuta, pamoja na wageni pia kuingia gharama kubwa kufika hifadhini.

Usafiri wa ndege nao ni miongoni mwa changamoto ambapo mara kadhaa watalii wanaotoka katika hifadhi nyingine zilizopo Arusha ingekuwa ni jambo jema usafiri wanaotumia uweze kufika hadi Kigoma, ikiwemo usafiri wa Mwanza kwenda Kigoma ambapo njia hiyo ikifunguliwa itachochea ongezeko kubwa la watalii.

Changamoto hiyo imekuwa ikichangia Hifadhi ya Gombe kushindwa kujiendesha na hivyo kutegemea hifadhi zingine kimapato na kubwa haswa inatokana na kukosa watalii wa kutosha kwa kila mwaka.

Bayona anasema, changamoto nyingine ni hifadhi kuwa jirani na maeneo ambayo hayana hali nzuri ya usalama ikiwemo nchi jirani kuwa na vita za hapa na pale na kusababisha kukosekana kwa usalama ndani ya hifadhi na hivyo watumishi kujitahidi kuwa makini kulinda usalama.

Sanjari na hilo ni ukosefu wa njia nyingi za kutokea endapo litaibuka tatizo ukizingatia amani katika nchi hizo bado ni ndogo, hivyo miundombinu ya barabara ingekamilika ingekuwa rahisi kuepuka majanga endapo yatajitokeza.

Mikakati

Mhifadhi Mkuu, Donatus Bayona anaeleza baadhi mikakati kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara kupitia Wakala wa Barabara (TANRODAS) ambapo kwa sasa wanaendelea na matengenezo kuelekea mpaka Kagunga.

“Lakini pia ujenzi huo pia utaanzia Mwandiga kuelekea Mwamgongo ambapo bado upembuuzi yakinifu haujafanyika kutokana na ukosefu wa fedha na endapo itakamilika itatoa fursa kwa watalii kufika kwa urahisi mkubwa hifadhini na hata gharama zinaweza kupungua kwa kiasi kikubwa,”anasema Bayona.

Mkakati mwingine ni kuboresha elimu kwa wananchi kuwalinda wanyama ambao wanatoka ndani ya hifadhi na kwenda vijijini, jambo ambalo wananchi wengi wamekuwa wakitoa taarifa licha ya kuwepo kwa wachache ambao bado hawana elimu ya kuwalinda wanyama.

Kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji kwa kutenga maeneo ya hifadhi ya msitu ili wanyama wakitoka nje ya hifadhi waendelee kupata malisho, lakini pia kutenga maeneo ya kilimo pamoja na maeneo ya shughuli zingine za kibinadamu hivyo kumekuwa na mipango ya kuboresha maeneo yaliyo nje ya hifadhi.

Pamoja na kuimarisha kitengo cha tiba kwa kuwa wanyama wamekuwa wakipata magonjwa ya kibinadamu, hivyo ni lazima kuwapatia matibabu na kabla ya hapo kumekuwa na utaratibu wa kuzuia magonjwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa mnyama kwa kuvaa maski midomoni.

Ambazo anasema, zinazuia magonjwa kama mafua kuwapata wanyama, lakini pia magonjwa yanayosambaa kwa njia ya hewa kutowapata wanyama na wageni.

Sanjari na hilo ni pamoja na kuzuia wageni ambao wanaumwa mafua kutopata fursa ya kuwaona wanyama hii yote ni kuzuia wanyama wasiweze kupata maambukizi ambayo yatawasababishia kuugua.