Na Yusuph Mussa,TimesMajira Online. Korogwe
WAKAZI wa Kijiji cha Gomba/Lamu Kata ya Makuyuni Tarafa ya Mombo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wametakiwa kutoacha kuzingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka kwa kuwa tishio la ugonjwa wa Corona halipo tena nchini.
Wametahadhariwa kwamba ugonjwa wa kipindupindu, kuhara kwa kawaida na kuhara damu, imekuwa ni sehemu ya magonjwa yanayosumbua wananchi wa Mkoa wa Tanga. Hivyo utamaduni wa kunawa mikono uliokuwepo wakati wa ugonjwa wa Corona, uendelee ili kuwaepusha wananchi na magonjwa ya mlipuko.
Hayo yamesemwa na Mtendaji wa Kijiji cha Gomba/Lamu, Cuthbert Kaale wakati akizungumza na Majira ambapo alisema baada ya wananchi kuitikia wito wa kufanya usafi kwa hiari yao wakati wa janga la Corona, wameona waendelee kutoa elimu na kuwachukulia hatua watakaokiuka kanuni na taratibu za usafi.
“Ni kweli wakati wa janga la Corona, wananchi walikuwa wanachukua tahadhari wenyewe kujikinga na ugonjwa huo, lakini baada ya kuona janga hilo limepita, wengine waliacha kufanya usafi. Hivyo baada ya kuona baadhi ya wenye migahawa na maduka ya dawa muhimu wameacha kuweka maji na sabuni, tumeona tuwachukulie hatua kwa kuwafikisha polisi na baadaye mahakamani,” amesema.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Gomba/Lamu, Mohamed Madinga amesema ugonjwa wa Corona uliingia Wilaya ya Korogwe, lakini kwenye kijiji hicho haukufika. Lakini wananchi wote walichukua tahadhari zote kujikinga na Corona. Na baada ya Corona kupita, sasa wanachukua tahadhari ya kupambana na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
“Ugonjwa wa Corona uliingia Wilaya ya Korogwe, lakini kwenye Kijiji chetu cha Gomba/Lamu haukufika, lakini kwa vile wananchi walianza kufanya usafi kwa kuweka ndoo za maji na sabuni, kulisaidia kupambana na magonjwa mengine kama kipindupindu. Ukiacha kipindupindu kikali cha mwaka 1978.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wiki iliyopita Ofisa Afya wa Mkoa wa Tanga, Jumanne Magoma amesema kipindupindu kilikuwa ni tatizo kubwa kwenye mkoa huo, ambapo mwaka 2008/09 watu 7,500 waliambukizwa ugonjwa huo.
Amesema kati ya hao, 103 walipoteza maisha na vifo vingi vilitokea Wilaya za Korogwe na Handeni. Huku mwaka 2015 watu 140 waliambukizwa kipindupindu na watatu walipoteza maisha.
Magoma amesema mwaka 2019, kulitokea mlipuko mwingine wa ugonjwa wa kipindupindu kwa watu 14 kupata ugonjwa huo na pia watu watatu walipoteza maisha.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi