Na Jackline Martin, TimesMajira Online
JUKWAA la Usawa wa Kijinsia (GEF) limekutana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kujadili namna bora ya kuharakisha upatikanaji wa vitambulisho vya taifa kwa Wanawake na watoto wa kike nchini.
Mkatano huo ulihusisha jumla ya wanachama 9 kutoka GEF na watendaji watano kutoka mamlaka ya vitambulisho vya taifa NIDA.
Pia Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi Benki Kuu ya Tanzania (BOT), jijini Dar Es Salaam hivi karibuni ambapo Mwenyekiti wa GEF, Angellah Kairuki alisema kitambulisho cha taifa ni hitaji muhimu kwa uwezeshaji wa wanawake na haki za kiuchumi.
“Mamlaka ya vitambulisho vya taifa nchini ni moja kati ya maeneo muhimu yatakayo Saidia katika kufikia usawa wa kizazi katika haki za usawa wa kiuchumi kwa kuwa kitambulisho cha taifa kinahitajika katika masuala mbalimbali ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na haki za kumiliki mali kama vile umiliki na usimamizi wa ardhi,” alisema Kairuki.
Pia Kairuki alisema wanawake na wasichana hawajafikiwa ipasavyo kuelewa umuhimu na mchakato wa hati hiyo ya kitaifa kabla ya ukombozi wao kamili kama ilivyobainishwa katika mpango wa GEF.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uzalishaji Vitambulisho kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Edison Guyai, alisema NIDA ndiyo msingi wa kila kitu hasa katika kujenga uchumi na kutoa huduma bora kwa mwananchi hivyo wamejipanga kuhakikisha wanasajili watu wote ambao wanatakiwa kusajiliwa na kufanya marekebisho ya sheria ili washushe umri kutoka miaka 18 na waanze mwaka 0 ili mtoto atakapozaliwa aweze kupata kitambulisho cha Taifa.
“Sheria ya NIDA inahitaji kusajili wananchi kuanzia miaka 18 na kuendelea hivyo sheria inahitaji kubadilishwa ili mamlaka iweze kusajili watoto tangu anapozaliwa na kuendelea”
Kuhusu NIDA kutambulisha Mfumo wa Usajili wa Watu kwa njia ya mtandao utakaowezesha wananchi wenye sifa za kuomba Vitambulisho vya Taifa kwa kujaza fomu mtandaoni mahali popote bila kulazimika kufika katika Ofisi za NIDA alisema bado wapo katika majaribio ambapo wanaufanyia tathmini hasa katika kuangalia mapungufu yanayopatikana kwa wananchi ambazo zitakuja kuboresha mfumo huu.
GEF ni programu ya miaka mitano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayonuia kufikia haki ya usawa wa kiuchumi kwa wanawake na wasichana ifikapo 2026 kama sehemu ya ahadi iliyojiwekea katika mkutano wa kimataifa ukiofanyika nchini ufaransa mwaka jana.
More Stories
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia
Kujenga ofisi ya kisasa,akipewa ridhaa ya Uenyekiti