Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Benki ya -KCB imefanikiwa kuhorodhesha hatifungani inayokidhi misingi ya sheria za kiislamu ijulikanayo kama “KCB Fursa Sukuk” katika soko la Hisa la Dar es salaam -DSE yenye thamani ya shilingi bilioni 11 ikiwa ni sawa na asilimia 110.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na dhamana Nicodemus Mkama wakati wa hafla ya kuhorodhesha hatifungani hiyo ambapo amesema mafanikio hayo yamechangiwa na Mazingira wezeshi ya uwekezaji Nchini.
“Mafanikio haya yametokana na mazingira wezeshi yanayotolewa na serikali ambapo katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia sheria ya fedha imeondoa kodi ya zuio kwenye hatifungani za kampuni kama ilivyo kwa hatifungani za serikali” Alisema Mkama na kuongeza kuwa
“Mafanikio haya yametokana na mazingira wezeshi ya kiutendaji ambapo mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana CMSA imeidhinisha kushusha kiwango cha chini cha ushiriki katika uwekezaji wa hatifungani ya fursa Sukuk kutoka shilingi milioni moja hadi laki tano hivyo kuwezesha ushiriki wa wawekezaji wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na wananchi wenye vipato tofauti, Taasisi na kampuni”
Aidha Mkama alisema mazingira wezeshi yanayotolewa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yamekuwa na matokeo chanya katika maendeleo ya sekta ya fedha hususan masoko ya mitaji ambapo thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji imeongezeka kwa asilimia 8.1 na kufikia shilingi trilioni 34.0 katika kipindi kilichoishia Desemba 2022, ikilinganishwa na shilingi trilioni 31.4 katika kipindi cha kilichoishia Desemba 2021.
Mbali na hayo, Mkama alisema fedha zilizopatikana kupitia mauzo ya hatifungani ya Sukuk zitatumika kuwekeza katika miradi inayokidhi misingi ya Shariah kupitia dirisha la KCB Sahl Banking ndani ya Benki ya KCB.
kwa upande wake Mkuu wa KCB Sahal Banking, Amour Muro alisema Upatikanaji wa fursa Sukuk katika soko la DSE utawapa fursa zaidi wawekezaji kwani wataweza kuuza hisa zao kwa wawekezaji wengine ambao hawajanunua au kununua hisa kutoka kwa wawekezaji wenza.
Aidha Muro alisema tangu kuanza kwa fursa Sukuk mapokeo yamekua makubwa kutoka kwa watanzania na hatimaye kufikia kuvuka lengo ambapo ilivutia wawekezaji wenye thamani ya Tsh.Bilioni 11 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 ya kiasi kilichotolewa cha Shilingi bilioni 10.
More Stories
Rais Samia kuzindua mfuko wa kuendeleza kazi za wabunifu
Makalla ampongeza Lissu kukiri CHADEMA haina wagombea Serikali za Mitaa
Chande azindua misheni ya uangalizi uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika