December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Furaha Fm yarudisha tabasamu kwa watoto waliokuwa wakiishi mazingira magumu,yatima.

Na Mwandishi wetu, Timesmajira,Dar es Salaam

WATOTO waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu na yatima wamepatiwa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo fedha kwa ajili ya umeme, nauli za shule pamoja na fedha wa ajili ya mfuko wa elimu kutoka kwa Aliyekuwa Mgombea wa Jimbo la Kawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Furaha Dominick

Akitoa Msaada huo Jijini Dar es salaam ,Dominick ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Furaha katika Familia iliyoamua kulea watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu iliyopo Kimara Suka pamoja na Kituo cha Kulelea Watoto yatima cha New Faraja Orphanage Center kilichopo Magomeni Jijini Dar es salaam.

Amesema alipokuwa mtoto aliwahi kuishi katika mazingira magumu akiwa na umri wa miaka mitatu hivyo amekuwa na utaratibu wa kumshukuru Mungu kupitia njiaa kuwa karibu na watoto hao.

“Mimi katika maisha yangu nimekuwa nikipenda kujitoa katika jamii ,maisha yangu yamekuwa ya namna hii kama njia ya kumshukuru Mungu kwa kila kitu”amesema Dominick.

Pia alimpongeza Mlezi wa familia iliyoamua kuishi na watoto waliokuwa wakiishi mazingira magumu na yatima kwa kuweza kuwalea watoto 60 katika nyumba mmoja na kuwachukulia kama sehemu ya familia

Kwa upande wake mlezi wa familia iliyoamua kuishi na kuwalea watoto waliokuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatarishi Dkt Consoler Eliya ameushukuru uongozi wa Redio Furaha kwa kuamua kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali .

“Naupongeza Uongozi wa Furaha Redio. Kwa kuamua kuja kuwatembelea watoto hawa na kutoa msaada hii imeonesha upendo mkubwa kwa watoto hawa tunashukuru sana kweli furaha Redio imeonesha furaha “amesema Dkt Consoler

Aidha amesema amekuwa akiishi katika nyumba moja na watoto 58 kutoka katika mazingira magumu na yatima pamoja na watoto wake wa kuwazaa wawili kama sehemu ya familia moja

“Nimekuwa nikikaa na watoto hawa kama familia sehemu ya familia yangu tunaishi Kwa upendo na amani …huduma hii niliianzisha miaka 19 iliyopita kwa kweli namshukuru Mungu kwa maisha ambayo tumekuwa tukiishi”amesema

Katika Kituo cha New Faraja Orphanage Center kilichopo Magomeni Dominick alipata fursa ya kula chakula pamoja na watoto hao kama ishara ya kuwaonesha upendo na kuwajali.

Mbali na kula chakula pia watoto hao waliopo katika kituo hicho walimuombea dua maalumu kwa Mkurugenzi wa Furaha Redio Dominick na kumshukuru kwa moyo wake wa kujitoa kwa ajili yao.

Naye Mkurugenzi New Faraja Orphanage Center Zamda Kishumba ameushukuru uongozi mzima wa Furaha Redio kwa kuwajali na kuamua kuungana nao na kula chakula pamoja.

Amesema kituo hicho kinawatoto 85 na kimekuwa kikiwalea katika mazingira mazuri ikiwemo kuwapatia elimu.