January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Filamu ya The Royal Tour, Reli ya SGR yachangia ongezeko la idadi ya watalii Hifadhi ya Taifa Mikumi

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kutokana na filamu ya “Tanzania the Royal Tour” na uwepo wa Reli ya mwendokasi SGR, idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi imeongezeka kutoka 54,021 mwaka 2019/2020 mpaka kufikia watalii 138,844 mwaka 2023/2024 huku akiwataka wawekezaji na wananchi kuongeza nyumba za wageni.

Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara leo Agosti 4, 2024 katika eneo la Round About ya Mikumi Mkoani Morogoro.

Ameongeza kuwa kwa sababu Serikali inaenda kujenga miundombinu kuunganisha jimbo la Mikumi na majimbo mengine na Wilaya nyingine, wakazi wa eneo hilo wategemee wageni wengi na wageni hao wanahitaji sehemu za kulala.

“Kwa upande wa utalii royal tour, hii imekuza utalii Tanzania yote hivyo sasa ni kuhakikisha watalii wanapita kwenye miundombinu mizuri na kufikia kwenye hoteli nzuri, pongezi kwa jimbo hili na Kilosa kwani imepita reli ya kisasa hivyo itumieni vyema kwani italeta wageni wengi zaidi”

“Ni matarajio yangu kwamba wageni watakuja kwa wingi sana hivyo wawekezaji na wananchi wazidi kuongeza ujenzi wa nyumba za wageni
Kwasababu tunakwenda kuongeza miundombinu basi mtegemee wageni wengi na wageni hawa wanahitaji pa kulala”

Katika hatua nyingine Rais Samia amesema mipango ya Serikali ni kufungamanisha reli ya TAZARA na SGR kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa na watu na kuleta maendeleo zaidi.

“Tutarekebisha miundombinu yote iliyoharibika na kuiweka kwenye kiwango kizuri zaidi” Alisitiza

Pia Rais Samia amesema serikali ina mpango wa kuendeleza bonde la ruhembe ambapo tayari wametenga Bilioni 7.2 na wanakwenda kufanya utafiti mwanzo hadi Mwisho wa Mbuga ya Mikumi lengo ni kujenga mabwawa na kingo zitakazodhibiti mafuriko ili lizalishe mara mbili kwa mwaka yaani mpunga na miwa na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi katika sekta ya kilimo.

“Hatutaki kusikia tena masuala ya mafuriko upande huu wa Tanzania “

Kwa upande wa REA Rais Samia amesema vimebaki vijiji vinne kupata umeme na hivyo kazi iliyobaki ni kupeleka umeme kwenye vitongoji hivyo.

Kutokana na hivyo Rais samia amewaomba wakazi wa maeneo hayo kutumia umeme kwa maendeleo yao binafsi kwa kufanya miradi midogomidogo itakayowapa kipato

Kadhalika, Rais samia amesema wanaendeleza na kukijenga vizuri kituo cha utafiti cha KATRIN na wamekipa kazi ya kuzalisha miche ya miwa ambayo wanakuja kuigawa bure kwa wananchi.

Amesema mikumi ni wazalishaji wazuri wa mpunga ambapo serikali itaangalia pale watakapojipanga watakwenda kwa kiasi gani kutoa mbegu ya mpinga

“Tunajua kwamba Kero haziwezi kuisha kwa wakati Mmoja lakini kwa kiasi kikubwa tupunguze adha kwa wananchi, tuwafanye wananchi waishi maisha ambayo wanastahili kuishi, kuwe na umeme, maji, hispitali za kisasa, shule nyingi n.k”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amesema wameielekeza Halmashauri, viongozi na Madiwani kwamba watambue kuweka viwanja vya uwekezaji ili wananchi washauhudie uwekezaji mkubwa unaotokana na utalii kama inavyotokea kwenye maeneo mengine.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi, Denis Londo amesema Mikumi ni mji wa kitalii ambapo bilioni 300 zimewekwa kwaajili ya kuboresha utalii ambao utaenda kuunganisha hifadhi ya nyerere na Mikumo na udzugwa

“Fedha hizi zinaenda kuboresha maisha ya wanachi wako wa hapa mikumi “

Londo alimuomna Rais Samia kupitia filamu ya Royal Tour aweze kufika mikumi na kuifanya filamu nyingine kama hiyo ili kuendelea kuongeza watalii wengi zaidi nchini