Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) William Erio amewahakikishia wawekezaji kutoka nje wanaokuja kuwekeza nchini Tanzania kwamba watakua salama katika kufanya biashara na uwekezaji kwa kutokuwa na bidhaa bandia
Erio ameyasema hayo leo jijini Dar es Salam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na wiki ya kudhibiti bidhaa bandia Duniani ambayo huadhimishwa kati ya mwezi juni na julai kila mwaka ambapo alisema serikali ya awamu ya sita imekuwa ikihimiza wawekezaji kutoka nje kuja nchini ili kufanya uwekezaji.
Kutokana na hivyo, Erio amewataka wananchi kuacha mara moja matumizi ya bidhaa bandia na badala yake kuhakikisha kuwa wanatumia bidhaa halisi hali itakayosaidia kuchochea uwekezaji, kukuza fursa za ajira na hatimaye kuchagiza ukuaji wa uchumi wao na taifa kwa ujumla.
“Uzuri wake kusiwe na bidhaa bandia ili wale wanaokuja kuwekeza wakija kufanya tathmini yao ya bidhaa gani waje wawekeze na kwa kiwango gani waje wawekeze wakija kwenye utendaji wakutane kwamba hali halisi inashabihiana na matokeo ya stadi walizozifanya Kwasababu hakutokua na biashara ya bidhaa bandia na wawekezaji watakuja wengi zaidi”
Erio amesema kuwa kati ya asilimia 2.5 na 3.5 ya biashara zinayofanyika ulimwenguni zinahusisha bidhaa bandia ambapo amebainisha baadhi ya madhara ya bidhaa hizo kuwa ni kutopata thamani halisi ya fedha pamoja na madhara mbalimbali ya kiafya kwa watumiaji
“Wiki ya kudhibiti bidhaa bandia duniani , wiki hii inaadhimishwa sehemu zote duniani kati ya mwezi wa 6 na 7 na sababu yake ni kwamba bidhaa bandia zina matatizo mengi lakini katika biashara zinazoendelea sehemu mbalumbali duniani kati ya asilimia 2.5 na 3.5 ya biashara yote inayofanyika duniani inahusisha bidhaa bandia”
“ Bidhaa bandia zina matatizo hata katika maeneo ya kiuchumi kwanza linaathiri ubunifu kwasababu katika kushindana unatakiwa kila kitu uje na kitu kipya, Kuwa na na bidhaa katika uchumi kunadhorotesha biashara kwasababu pamoja na mambo mengine biashara ya bidhaa bandia inafanyika katika mifumo isiyo rasmi haifuati mifumo ya rasmi ya serikali kwahiyo kuna kodi, ubora wake ni wa chini”
Erio amewataka wadau kuendelea kuungana nao katika kuendelea kutoa elimu kuhudu matumizi ya bidhaa feki ili kuendelea kukuza uchumi nchini
Kilele cha maadhimisho hayo yaliyobebwa na Kauli mbiu isemayo “Kudumisha uhalisia kwa kulinda ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi nchini” kinatarajiwa kuwa julai 18 katika ukumbi wa mikutano ya mlimani city jijini dar es salaam ambapo kutaambatana na maonyesho mbalimbali ya wajasiriamali na wamiliki wa viwanda vidogovidogo pamoja na majadiliano ya jopo.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja