Na Jackline Martin, TimesMajira Online
TUME ya Ushindani Tanzania (FCC)
na vyombo vingine vinavyosimamia masuala ya biashara, vimetakiwa
kuendelea kutekeleza majukumu yao
kwa kuongeza nguvu ya utoaji elimu
kwa wafanyabiashara ili kuepusha
uvunjaji wa sheria.
Agizo hilo alilitoa jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani yaliyofanyika jana kwa Kaulimbiu isemayo; ‘Njama baina ya washindani na madhara yake’
“Tuendelee kutoa elimu kwa wazalishaji wenyewe, lakini pia kwa walaji ili tuendelee kuelewana juu ya athari kubwa za kufifisha ushindani ndani ya Taifa letu,” Alisema Dkt. Kijaji na kuongeza;
“Mbinu ambazo siyo halali zina athari
hasi, huwa wakati mwingine tunafikiria ni athari hasi kwa watumiaji, lakini muda mwingine hata kwako wewe mfanyabiashara au mzalishaji zile mbinu ambazo Si halali zinaweza kukunufaisha
kwa muda mfupi, lakini kwa mudabmrefu zinaweza zikakuharibia soko, Lazima Sheria ziwepo ili zisimamie vitendo hivi visiwepo, kwani vinatuathiri sisi wenyewe”.
Dkt. Kijaji aliwataka wawakilishi wa wadau wafahamu kuwa madhumuni ya serikali ya awamu ya 6 katika kusimamia uchumi wa soko, si kikataza biashara bali ni kutaka ifanyike kwa kuzingatia sheria na misingi ya ushindani.
“ Washindani wanatakiwa kushindana kwa uhuru na amani na si kula njama za kukwepa kushindana sokoni ili kutimiza malengo yaliyowekwa na sheria ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma iliyo bora,”alisema.
Waziri Kijaji alisema sheria ya ushindani ina umuhimu mkubwa sana katika kujenga uchumi wa Taifa, hivyo wafanyabiashara wanapofanya biashara zao kwa kufuata misingi ya sheria wataweza kuongeza ufanisi katika uzalisha na usambazaji wa
bidhaa na huduma.
“Faida hizi zitatufanya tuweze kushindana katika masoko ya kikanda na Kimataifa ikizingatiwa kuwa tayari Taifa letu lipo katika masoko mbalimbali ya kikanda , tupo kwenye soko la Afrika Mashariki, soko la SADC na soko la eneo huru la biashara Afrika,” alisema.
“Bila kufuata misingi hii ya ushindani
ni wazi Taifa letu linaweza kuwa soko la bidhaa za wenzetu,” alisema
Waziri Kijaji alisema kukosekana kwa ushindani ndani ya soko hudumaza ukuaji wa uchumi kwani wawekezaji wengi huvutiwa kuja kuwekeza nchini, hivyo ni vyema kushirikiana ili fursa zilizopo nje ziweze kuletwa katika soko la ndani.
Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) William Erio alisema Msingi wa kuadhimisha siku ya ushindani Duniani ni kutekeleza adhimio la baraza kuu la umoja wa mataifa katika kikao chake cha mwezi April 1980 ambacho kilipitisha taratibu na kanuni za kudhibiti vitendo vinavyofifisha ushindani katika biashara ulimwengu.
“Katika kutekeleza kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha maadhimisho haya tumetekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kufanya mikutano na waandishi wa Habari lakini pia semina mbalimbali kuhusu uelewa wa masuala ya ushindani, tumetoa elimu kwa umma kuhusu majukumu ya FCC na maadhimisho ya siku hiu katika Kanda 4 nchini “
Erio alisema kupitia mikutano hiyo walipokea mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wadau na ambapo mapendekezo hayo watayafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu za kiserikali.
Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI), Bw. Leodgar Tenga alisema wafanyabiashara hawana budi kufanya biashara zao kwa kufuata sheria za ushindani kwani kwa kufanya hivyo mlaji na mtumiaji ataendelea kufaidia kwa kupata bidhaa na huduma bora katika bei inayo aksi uhalisia.
Aidha Tenga alisema kwa mfanyabiashara itamsaidia kupata ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma lakini pia kukuza ubunifu vitu vitakavyopelekea kukua kwa uchumi wa nchi.
“Uwepo wa sheria ya ushindani imeleta faidha nyingi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi kupitia muunganiko wa Makampuni hivyo kuongeza pato la Taifa na ajira kwa wananchi”
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM