Na Mwandishi wetu, Timesmajira
ZAMBIA. Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Bodi ya Udhibiti wa Nishati Zambia (ERB) wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kimiundombinu ili kuboresha huduma za nishati katika nchi zao.
Wakati wa kikao baina ya Bodi hizo, zilizokutana leo, tarehe 24.03.2025 katika Ofisi za ERB Lusaka, imebainishwa kuwa hivi karibuni Taasisi hizo mbili zitasaini hati ya makubaliano kwaajili ya ushirikiano huo.
Baadhi ya maeneo ambayo EWURA na ERB watashirikiana ni pamoja na kubadilishana taarifa za kitaalamu, kiuchumi na kimiundombinu, kujengea uwezo wataalamu, na kubadilishana uzoefu katika masuala ya kitaalamu.

Akizungumza wakati wa kikao hicho,
Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA, Prof. Mark Mwandosya, amesema kuwa ushirikiano kati ya EWURA na ERB tayari umeleta mafanikio makubwa katika udhibiti wa sekta za petroli, gesi asilia, na umeme. Aliongeza kuwa ushirikiano huo umechangia kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya usalama, mifumo ya kisheria, na ufanisi katika uendeshaji wa sekta hizo.

“Moja ya mafanikio makubwa ya ushirikiano wetu ni juhudi za pamoja katika ukaguzi wa bomba la mafuta la TAZAMA. Ukaguzi huu haujaimarisha tu usalama na ufanisi wa miundombinu hii muhimu, bali pia unadhihirisha dhamira yetu ya kuendeleza ubora wa udhibiti katika ukanda huu,”
amesema Prof. Mwandosya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB ,James Banda amesema kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya sekta wanazosimamia na kusisitiza kuwa kusainiwa kwa hati ya makubaliano kutatoa msukumo zaidi katika kuboresha huduma za nishati na kuimarisha ufanisi wa kiutendaji.
More Stories
Prof.Muhongo achangia mifuko 250 ya saruji ujenzi shule ya sekondari Nyabakangara
Child support Tanzania yapongezwa kutetea maslahi watoto wenye ulemavu
Tanzania yaadhimisha siku ya hali ya hewa,kwa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu ya hali ya hewa na usambazaji wa huduma zake.