March 21, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ETDCO wakamilisha mradi wa Kilovolti 132 Tabora – Urambo

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO) imefanikiwa kuwasha rasmi laini ya msongo wa Kilovolti 132 yenye mrefu wa kilomita 115 kutoka Tabora hadi Urambo ambao unakwenda kuwasaidia
wananchi wa Urambo na Kaliua kupata umeme wa uhakika na
kuchochea maendeleo.

Akizungumza leo Machi 20, 2025 Mkoani Tabora katika zoezi la kuwasha laini hiyo mpya ya Tabora hadi Urambo, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya ETDCO CPA. Sadock Mugendi, ameishukuru Serikali pamoja na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuwaamini kutekeleza mradi huo, huku akieleza kuwa wananchi wa Wilaya ya Urambo na Kaliua wategemee kupata umeme wa uhakika.

CPA. Mugendi amesema kuwa mradi huo umetekelezwa na watalaamu wazawa jambo ambalo limeonesha wanaweze kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati bila tatizo lolote.

Meneja wa Mradi wa Tabora- Katavi kwa upande wa TANESCO Mhandisi Sospeter Oralo, amesema kuwa mradi huu umegharimu shilingi billioni 40, ambapo gharama ya laini yenye msongo wa Kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Urambo ni bilioni 24, huku ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Urambo zimetumika bilioni 16 fedha ambazo zimetoka serikali ya Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Ufundi ETDCO Mhadisi Dismas Massawe, amesema kuwa baada ya kuwasha laini hiyo wananchi wa Urambo na Kaliua watarajie kupata umeme wa uhakika kupitia kituo cha Uhuru Wilaya urambo chenye mashine umba (transformer) ya Megawatts 28.

Nae, Meneja wa Mradi wa Tabora hadi Urambo upande wa ETDCO Mhandisi Ntuli Burton, amesema kuwa mradi huu ulianza April 2024 na tulitegemea kumalizika June 2025. “Tunashukuru Mungu tumefanikiwa kumaliza mradi huu kabla ya wakati ili wananchi wa Urambo waweze kupata umeme wa uhakika haraka iwezekanavyo”.

Kupitia mradi huo wa kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi Urambo wenye msongo wa kilovolti 132 utasiadia kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Urambo, Kaliua pamoja na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.