Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online. Morogoro
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuepuka majungu, fitina na makundi katika maeneo ya kazi na badala yake, kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta ufanisi na tija kwa mamlaka hiyo na taifa.
Akizungumza katika kikao cha 29 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika mkoani Morogoro, Waziri huyo amewasisitiza wafanyakazi hao kushirikiana katika kupinga vitendo vya wizi na rushwa kwa kufanya kazi kwa weledi, bidii pamoja na kulinda kwa nguvu zote mahusiano mema baina yao.
“Ni imani yangu kwamba katika kutekeleza majukumu yenu mliyopewa na serikali, mtaendeleza utaratibu wa kushirikiana kati ya menejimenti na chama chenu cha Wafanyakazi (DOWUTA), kulinda maslahi ya taifa ndani ya bandari kwa kupinga vitendo vya rushwa na wizi,” amesema.
Ameongeza kuwa, kila mmoja anatakiwa kuheshimu nafasi ya kila mtu katika eneo la kazi kwani majukumu yao yanategemeana kwenye kufikia malengo ya mamlaka hiyo.
Amewasisitiza Wajumbe wa Baraza hilo kutumia kikao hicho kupitia kwa makini mpango na bajeti yao, kushauri na hatimaye kuja kusimamia utekelezaji wake.
Ameitaka Menejimenti na wawakilishi wa DOWUTA, kuwajibika kwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wa mamlaka, wanatambua na kutimiza wajibu wao ipasavyo pamoja na kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Erick Hamisi amesema atashirikiana na wafanyakazi wa mamlaka hiyo ili kufikia malengo ya taasisi waliyojiwekea.
Kikao hicho cha 29 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPA, kina dhima kuu ya kujadili masuala ya bajeti, utendaji, uendeshaji wa bandari na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na mamlaka.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM