November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

EAC kuweka mpango mkakati wa kuendeleza soko la Bima

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki-EAC zimedhamiria kuweka mpango mkakati wa kuendeleza soko la Bima na kukuza uelewa wa Bima kwa wananchi wa nchi hizo.

Mpango huo wamekubaliana kuuzindua mwaka 2024 nchini Kenya ambapo Kamishna wa Kenya atakuwa Mwenyeji wa Mkutano huo.

Hayo yamesemwa Jana Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Bima nchini – TIRA, Dkt. Baghayo Saqware katika Mkutano wa Makashna na viongozi wa Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa Bima katika Jumuhiya za Afrika Mashariki waliokutana kwa siku Tano kujadili njia Bora ya kuendeleza Sekta ya Bima katika nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuona namna ya kuwawezesha raia wake kuwa na mwitikio mkubwa wa matumizi ya Bima.

Amesema kwenye mpango wa kitaifa wa fedha wanahitajika kuwa na watanzania zaidi ya asilimia 50 ambao wanatakiwa kutumia huduma na bidhaa za Bima.

“Mbali na mpango mkakati ulioanza mwaka 2019 na kutarajiwa kumalizika mwama 2024, bado tunampango mpya wa kuendeleza soko la Bima kuanzia mwaka 2024-2030 ambapo kwenye mpango wa kitaifa wa fedha tunahitajika kuwa na watanzania zaidi ya asilimia 50 ambao wanatakiwa kutumia huduma na bidhaa za Bima.”

Amesema mkutano huo ambao nchi ya Kenya, DRC Congo, Rwanda, Uganda na Tanzania wameshiriki ni wa 19 na kueleza kuwa wanaendelea kutekeleza mpango wa kuendeleza soko la Bima mwaka hadi mwaka.

“Mkutano huu wa makamishna na viongozi wa Mamlaka zinazohusika na usimamizi wa Bima katika Jumuhiya za Afrika Mashariki, ni mkutano wa 19 na sisi Tanzania tumepata Bahati ya kuwa wenyeji, tumekuwa hapa kwa muda wa siku Tano tunawashukuru sana kwa ujio wa mkutano huu”

“Kwenye mkutano huo tumejadili mpango wa East Africa na katika mpango huo tumeangazia maeneo mengi namna ya kuongeza uelewa, idadi ya watu wanaotumia huduma za Bima, lakini pia namna ya kutumia fursa za kidigitali kusambaza huduma za Bima kwa wananchi wote wa East Africa” Amesema

Aidha Dkt. Saqware amesema Katika mkutano huo wamejadili maendeleo ya Sekta ya Bima katika jumuiya ya Afrika Mashariki na kuangazia maeneo ya vihatarishi vya Bima kidigitali na maendeleo ya Bima ya afya.

Mbali na hayo, Dkt. Saqware amesema Ushirikiano wa kikanda kwenye magari ya mizigo yanayokwenda nje ya nchi umejadiliwa, namna bora ya kuendesha biashara hiyo lakini pia kuangalia namna ya kutoa fidia kwa watu ambao wanaumizwa na magari ambayo yanapita kama transit nchini Tanzania.

Kuhusu changamoto, Dkt. Saqware amesema masoko ya East Afrika yana changamoto zinazolingana ikiwemo ‘Penetration’, uelewa, mtazamo wa wananchi kuhusu Bima lakini pia changamoto ya kuhakikisha kuwa bima inawafikia Kila mtu.

Hivyo Dkt. Saqware amewataka watoa huduma wote kuendelea kubuni huduma sahihi kwa wananchi wa Tanzania lakini pia wananchi waendelee kununua bidhaa na huduma za Bima kwaajili ya kujikinga kutokana na mali, afya na maisha

“Huduma hizi zinatoka fursa za uwekezaji hivyo tutembelee Makampuni ili kuona mnaweza kununua bidhaa gani ya Bima”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bima kutoka nchini Kenya, Godfrey Kiptum amesema changamoto kubwa iliyopo katika nchi za Afrika Mashariki ni uwepo wa idadi ndogo ya watu wanaotumia Bima hivyo amewahamasisha wananchi wote wa Afrika Mashariki kutumia Bima za Maisha.