Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WANANCHI wametakiwa kutumia mfumo wa kupokea maoni, malalamiko au pongezi Serikalini (e-Mrejesho), ili kuwasilisha maoni yao na Serikali iweze kuyafanyia kazi kwa wakati.
Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) Mhandisi Benedict Ndomba, wakati akizungumza na waandishi wa Habari katika ofisi za Mamlaka jijini Dodoma.
Ndomba amebainisha kwamba, mfumo wa e-Mrejesho ambao hivi karibuni umeshinda tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Ubunifu katika Huduma za Umma kwa mwaka 2024 ‘UN Public Service Innovation Awards’ unadhihirisha kuwa ni kiungo muhimu cha mawasiliano kati ya serikali na wananchi .
“e-Mrejesho umetambuliwa kimataifa kama jukwaa linalowezesha serikali kukusanya maoni na malalamiko ya wananchi kwa njia ya kidijitali, na hivyo kufanya maamuzi ya sera na utekelezaji kwa wakati.” Ameeleza Mhandishi Ndomba.
Ameongeza kuwa, Tanzania ilikuwa moja kati ya nchi mbili tu za Afrika zilizotunukiwa tuzo hiyo, nyingine ikiwa ni Afrika Kusini kati ya nchi 73 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoshiriki, ambapo mifumo 400 iliwasilishwa wakati mifumo 15 pekee ndiyo ilishinda tuzo mbalimbali ukiwemo mfumo wa e-Mrejesho.
Amesema, tuzo hizo za Umoja wa Mataifa kuhusu Huduma za Umma zinalenga kuhamasisha ufanisi, uwazi na ushirikishwaji katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, na kuthamini mchango wa taasisi za umma katika kukabiliana na mahitaji ya kijamii, kiuchumi na mazingira ya jamii.
“Mfumo wa e-Mrejesho unasaidia kuongeza uwajibikaji, kwani lalamiko linapofika kwenye taasisi litaonekana kwenye ngazi zote za uongozi wa taasisi hiyo na kila Afisa, aliyelifungua ama kulifanyia kazi ataonekana”, amesema Ndomba na kuongeza kuwa,
“Pia mfumo huu unafanya uchambuzi wa taarifa na kumuwezesha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais UTUMISHI na Katibu Mkuu Kiongozi kuona malalamiko yaliyowazi, yanayoshughulikiwa na yale yaliyokamilika”.
Kuhusu utambulisho wa mtoa malalamiko katika mfumo wa e-Mrejesho, Mhandisi Ndomba amebainisha kwamba mfumo haumlazimishi mwananchi kuandika taarifa zake binafsi kama jina au anuani yake au namba ya simu.
“Siyo lazima kuandika jina lako kama hutaki kufanya hivyo, lakini ni muhimu kuandika taarifa zako ili maoni au malalamiko yako yanapofanyiwa kazi upate majibu yake kwa haraka zaidi.” Amesema Mhandisi Ndomba
Machi 13 mwaka huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, aliwataka viongozi wa umma kutumia Mfumo e-Mrejesho ili kupokea maoni ya wananchi kuhusu Serikali na pia kutoa mrejesho kwa wananchi kupitia mfumo huo ili kuimarisha uwajibikaji kwa viongozi wa umma.
Mfumo wa e-Mrejesho unapatikana kwa njia tatu ambazo ni kupitia simu ya mkononi kwa kubofya *152*00# na kisha kuchagua namba 9 na kisha namba 2, njia zingine ni kupitia simu janja kwa kupakua Aplikesheni (Mobile App) ya e-Mrejesho inayopatikana kwenye Play Store na Apple Apps Store, na kwa njia ya Tovuti ya emrejesho.gov.go.tz.
Mfumo wa e-Mrejesho umesanifiwa na kutengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), unasimamiwa na kuendeshwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili