November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

e-GA yatekeleza agizo la Rais Samia mfumo wa GoVESB

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

MAMLAKA ya Serikali Mtandao(e-GA),imesema imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma inaunganishwa na kubadilishana taarifa kwa kujenga mfumo mkuu wa ubadilishanaji taarifa serikalini(GoVESB).

Ambapo hadi sasa jumla ya taasisi za umma 109 zimeunganishwa katika mfumo wa GoVESB na mifumo 117 imesajiliwa na miongoni mwa taasisi hizo ni mamlaka ya vitambulisho vya Taifa(NIDA),wakala wa leseni za biashara (BRELLA),Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na zinginezo.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo Disemba 22,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao,Mhandisi Benedict Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa jitihada za mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali.

Mhandisi Ndomba amesema kuwa pamoja na agizo la Rais,mfumo huo umetengenezwa kwa kuzingatia kifungu cha 48(2)cha sheria ya serikali mtandao Na.10 ya mwaka 2019 kinachoitaka mamlaka hiyo kuanzisha na kuendesha mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa.

“GoVESB ni mfumo wa Kieletroniki unaounganisha mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma iweze kusomana na kubadilishana taarifa kila inapohitajika,”amesema.

Aidha Mhandisi Ndomba ametaja lengo la Mfumo huo ni kuziwezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali kwa usalama,kupunguza urudufu wa mifumo,kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda kwakuwa taarifa hupatikana kwa wakati.

Amesema kabla ya kuanza kwa mfumo wa GoVESB kulikuwa na changamoto mbalimbali za ubadilishaji wa taarifa katika taasisi za umma,zikiwemo kutumia muda mrefu kupata taarifa kwani taasisi zililazimika kuwasilisha maombi ya kupata taarifa inazohitaji kwa njia ya barua katika taasisi husika.

“Utaratibu huu wa barua ulichukua muda mrefu kupata taarifa hizo jambo lilichangia kupunguza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi,

“Changamoto nyingime ilikuwa ni utofauti wa utaratibu wa kupata taarifa kutoka taasisi moja hadi nyingine kwani kila taasisi inao Utaratibu wake wa ndani wa kupata na kutoa taarifa na wakati mwingine utaratibu hubadilika,”amesema Mhandisi Ndomba.

Ameeleza kuwa awali ili mifumo ya TEHAMA iweze kusomana ililazimika kuinganisha mfumo mmoja kuzungumza na mifumo mingine kila inapohitajika ambapo amesema uunganishwaji huo ulisababisha urudufu wa mifumo,kupungua kwa usalama,kupunguza ufanisi wa mifumo na kuongeza gharama za usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA.

“Kupitia GoVESB changamoto hizo zimetatuliwa na sasa taasisi zote zinabadilishana taarifa kupitia mfumo huu hupata taarifa zinazohitajika kwa wakati na kwa usalama zaidi,vilevile mfumo huu umesaidia kuokoa muda wa kuwahudumia wananchi lakini pia hupunguza gharama za kutengeneza mifumo midogo midogo ya TEHEMA inayounganisha na mifumo ya taasisi nyingine,”amesema Mhandisi Ndomba.

Vilevile Mhandisi Ndomba amesema kuwa e-GA imeshirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo TRA,TPA na Wizara ya fedha katika kusanifu mfumo wa pamoja wa Kieletroniki wa uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha (Tanzania Electronic Single Window System-TeSWS).

“Mfumo wa TeSWS ni sehemu ya utekeleza wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara nchini,mfumo ambao unawawezesha wafanyabishara kukamilisha maombi ya vibali na maandalizi ya malipo ya kodi za forodha kidijitali bila kwenda kwenye taasisi mbalimbali za udhibiti wa forodha hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,”amesema.

Pia amezungumzia ubadilishaji wa taarifa kati ya mifumo ya TEHAMA ya serikali na ya sekta binafsi ambapo amesema unawezeshwa kadri ya mahitaji yanavyojitokeza.