Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amesema katika kuhakikisha inaongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi kwa wakazi wa mji wa Dodoma imechimba visima vitano katika eneo la Nzuguni ambavyo vina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 7.6 kwa siku.
Aidha amesema,kufuatia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofanywa na mamlaka hiyo,inatarajiwa hadi ifikapo 2024 wamelenga kufikisha asilimia 93 ya upatikanaji ya huduma ya Majisafi na salama lakini pia kuongeza muda wa huduma kutoka saa 13 ya sasa hadi 19.
Akizungumza jijini Dodoma na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu na mikakati ya Mamlaka hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 Mhandisi Aron alisema,hatua hiyo inakwenda kupunguza uhaba wa maji kwa asilimia 11 kwa wakazi wa mji wa Dodoma.
“Moja ya eneo ambalo limekuwa na chnagamoto ya upatikanaji wa maji safi ni eneo la Nzuguni na ndiyo maana tukaamua kujenga mradi huo ambao sasa wakazi wa Nzuguni watatumia nusu tu ya maji yote yatakayopatikana na yanayobaki yanaenda kutumika maeneo ya jirani na hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo.”amesema Mhandisi Aron
Aidha amesema,katika kipindi cha Agosti mwaka huu wana mpango wa kuanza mtradi wa uchimbaji visima vingine vitano lengo likiwa ni kuendelea kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika mji wa Dodoma.
“Baada ya miradi hii yote kukamilika inawezekana Nzuguni ikawa na maji mengi kuliko maeneo mengine hapa Dodoma .”amesistiza
Alisema mpango mwingine ni kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ambapo alisema,Mamlaka hiyo inakwenda kuchimba kisima kingine eneo la Iyumbu ili kusaidia UDOM kupata huduma hiyo kwa uhakika.
“Tunataka kuongeza maji katika eneo la UDOM ambapo kwa sasa kuna watu takriban 35,000 na maji tunayoyapeleka ni wastani wa lita 70 kwa kila mtu kwa siku. kwahiyo tunatakiwa tuongeze mpaka lita 120 hapo ndipo chuo kitakuwa salama” amesema Aron
Pia amesema Mpango mwingine ni kuchimba visima vingine vya maji katika maeneo ya Nala,Michese na Vyeyula kwa ajili ya kuongeza maji yanayokuja katikati ya jiji, kwahiyo huo ndio mpango wa dharura unaokwenda kupunguza tatizo la maji.
“Miradi yote hiyo inakwenda kuhakikisha kwamba tunaongeza huduma ya maji kufikia asilimia 93% ndani ya mwaka 2024, na pia kuongeza muda wa huduma kutoka saa 13 ya sasa hadi 19.
.Alizungumzia kuhusu mradi wa miji 28 Tanzania Bara na visiwani imetengewa bilioni 17, na fedha hizo zinakwenda kuongeza matenki ya maji, visima vya ziada na pia zinakwenda kuhakikisha maeneo yote ya Chamwino yanapata maji.
“Kupitia fedha hiyo, chamwino inakwenda kupata maji kwa masaa 24 kwa asilimia 100% na inakuwa salama kwa miaka 30 ijayo” amesema
More Stories
Watumishi wa Mahakama waonywa
CCM ilivyotambua mchango wa wanahabari Mkutano Mkuu Maalum
Wasira :Uamuzi Mkutano Mkuu umezingatia katiba