January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DP World yaingia mkataba wa miaka 30 na serikali ya Tanzania

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

kampuni ya DP World imesaini
mkataba wa miaka 30 na Serikali ya Tanzania kuendesha na kuboresha maeneo mahususi ya Bandari
ya Dar es Salaam, na kuiunganisha Tanzania na masoko makubwa duniani.

Mkataba huo wa uendeshaji ulitiwa saini leo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, na Sultan Ahmed Bin Sulayem, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni
Tanzu za DP World, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Ukiainisha maeneo mahususi ya uwekezaji, mkataba huu wa uendeshaji na uboreshaji unalenga kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam kwenye usafirishaji na uchukuzi wa mizigo inayoingia na kutoka nchini Tanzania. DP World itaanza kwa kuwekeza dola milioni 250 kuboresha bandari, na uwekezaji unatarajiwa kufikia dola bilioni moja ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa maeneo mengine ya shughuli za bandari.

Uwekezaji huu utakuwa na faida kubwa kwa Tanzania hasa katika maeneo muhimu kama vile kutengeneza ajira na kuongeza urahisi wa kupata huduma na bidhaa, pamoja na mambo mengine.

Kwa uwekezaji huu, bandari ya Dar es Salaam itaunganishwa na maeneo mengine ya mbali kwenye eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kutumia mtandao wa barabara, reli, njia kuu za kupitisha mizigo (logistics corridors) na bandari nyingine, na hivyo kusaidia sana kupunguza pengo la mahitaji ya
huduma za uchukuzi barani Afrika na kuunganisha biashara za eneo hili na masoko ya dunia.

Kupitia mkataba huo wa uendeshaji, DP World itakodishwa gati namba 4-7, na kuruhusiwa kutoa huduma kwenye gati namba 0-3 katika bandari ya Dar es Salaam. Uwekezaji huu mpya utaimarisha
zaidi bandari hiyo ambayo katika miaka ya karibuni ilinufaika na jitihada za serikali ya Tanzania kuboresha bandari zake.

DP World itafanya kazi na TPA na wadau wengine wa bandari kuhakikisha kasi ya uondoaji wa mizigo bandarini inaongezeka na kwa utaratibu wa kisasa – ikizingatia upekee wa bandari ya Dar es Salaam
kama lango muhimu la usafirishaji (kwa njia ya maji) wa madini ya shaba kutoka Afrika ya Kati na Kusini kwenda kwenye masoko ya kimataifa.

Kuongezeka kwa ufanisi kutavutia meli nyingi na kubwa zaidi kutumia bandari ya Dar es Salaam; jambo litakalopunguza gharama kwa waagizaji na wasafirishaji wanaotumia bandari hiyo.

Vilevile, DP World itawekeza kwenye miundombinu ya kisasa kwenye bandari hiyo, ikiwemo uwekaji wa majokofu ili kusaidia wakulima na wafanyabiashara ya mbogamboga na matunda kuhifadhi bidhaa zao zisiharibike kabla ya kusafirishwa.

Zaidi ya hapo uwekezaji utaongeza urahisi wa kufikika kwa maeneo yanayotumia reli na yale yatakayotengwa kama maeneo ya uwekezaji ili kuboresha miundombinu na kuongeza ushawishi wa Tanzania kuvutia biashara duniani.

Akizungumza katika utiaji saini huo, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni Tanzu za DP World, Sultan Ahmed Bin Sulayem, amesema: “Ni heshima kubwa kwetu kushirikiana na Serikali ya Tanzania
kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam. Hatua hii inaendana na mipango ya kimkakati ya maendeleo inayopangwa na Tanzania na ni uthibitisho wa uongozi mahiri wenye maono wa Mheshimiwa Rais
Samia Suluhu Hassan. Jambo hili litatoa fursa nyingi kwa eneo hili la Afrika kwa kuliunganisha na masoko ya dunia, kutengeneza ajira nyingi zaidi, kuongeza upatikanaji wa huduma na bidhaa, na
kuongeza tija kwa wadau wote. Mkataba huu ni mwendelezo wa dhamira ya DP World kuunganisha watu na biashara kwa lengo la kukuza uchumi wa dunia. Pamoja na bandari nyingine tunazofanya nazo
kazi, uwekezaji huu ni hatua nyingine kwenye jitihada zetu pana za kushirikisha wataalamu wetu wa kimataifa na wazawa wa nchi husika kukuza mnyororo wa usafirishaji ili kukuza uchumi wa bara zima
la Afrika”.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema: “Kusainiwa kwa mkataba huu baina ya Serikali ya Tanzania na DP World ni tukio kubwa kwa sababu unatupa uwezo wa kujenga miundombinu
ya kisasa kwa kutumia ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi. Kwa kutumia utaalamu wa DP World, bandari hii itakuwa chachu ya kusababisha kupatikana kwa ajira za moja kwa moja na nyingine
kupitia sekta kama vile usafirishaji, usambazaji na mnyororo mzima wa sekta hii. Kikubwa zaidi, Mamlaka ya Bandari (TPA) itamiliki hisa kwenye kampuni itayotekeleza uwekezaji huu bandarini, na
hakutakuwa na ajira yoyote itakayopotea.”

Kwa upande wake, akizungumza katika tukio hilo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari za Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema: “Tuna furaha kubwa kushirikiana na DP World kwenye
uboreshaji wa bandari ya kimkakati ya Dar es Salaam. Mradi huu utaongeza tija kwa watumiaji na kuisaidia serikali katika lengo lake la kupunguza gharama za usafirishaji. Mradi huu wa kimkakati ni ushahidi wa uwezo wetu wa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kwa kushirikiana na wabia wetu, na hivyo kuipa serikali nguvu ya kutumia fedha zake kwenye sekta nyingine zenye uhitaji zaidi”.

DP World inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kufikia malengo yake ya kimkakati barani Afrika yanayolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwezesha biashara na kuunganisha masoko kwenye mtandao wa dunia.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari (TPA) Plasduce Mbossa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu wakitia saini Mkataba wa upangishaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam pamoja baina ya Kampuni ya DP World ya Dubai iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Sultan Ahmed bin Sulayem kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu akipongezana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DP World ya Dubai Sultan Ahmed bin Sulayem mara baada ya kusaini Mkataba wa Uendeshaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TPA Mhe. Balozi Ernest Mangu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya DP World ya Dubai Sultan Ahmed bin Sulayem, wakionesha Mkataba wa Upangishaji wa Gati namba 4 mpaka 7 za Bandari ya Dar es Salaam mara baada ya kusaini Mkataba huo kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 22 Oktoba, 2023.