Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online, Mbeya
WANANCHI wa Kata ya Mwakibete, Mtaa wa Bombambili katika Jimbo la Uyole jijini Mbeya wamejitolea kujenga barabara iliyokuwa kero kutokana na kuwepo kwa mto unaokatiza eneo hilo, hali iliyokuwa ikisababisha ugumu wa mawasiliano ya kijamii na shughuli za kiuchumi hasa nyakati za mvua na kiangazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi na wadau wa maendeleo kuamua kuungana na kuanza juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara inayounganisha maeneo ya Bombambili katika Jimbo la Uyole na Mbeya Mjini.
Akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi huo Albert Mwantongo amesema licha ya changamoto mbalimbali walizokutana nazo, wananchi wamefanikiwa kuanza kazi ya ujenzi kwa kutumia fedha zilizokusanywa kupitia michango ya wadau wa maendeleo pamoja na wakazi wa eneo hilo.

Kwa upande wake, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Uyole, Dkt. Tulia Ackson, amewapongeza wananchi na wadau wa maendeleo kwa jitihada zao za kuboresha miundombinu hiyo muhimu.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Dkt. Tulia amechangia malori 10 ya mawe pamoja na mifuko 100 ya saruji na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha barabara za maeneo hayo zinaboreshwa.
“Nitaendelea kufuatilia maeneo yote korofi ya barabara zetu ili yawe katika hali nzuri na kurahisisha shughuli za kiuchumi za wananchi, sambamba na kuendelea kuwaunga mkono,” amesema Dkt. Tulia.
Naye Diwani wa Kata ya Mwakibete, Lucas Mwampiki, amemshukuru Dkt. Tulia kwa mchango wake mkubwa katika kusukuma maendeleo ndani ya kata hiyo na Jimbo la Uyole kwa ujumla.
“Niwapongeze sana wananchi na wadau wa maendeleo kwa mshikamano wenu na kuweka kipaumbele miradi ya maendeleo. Hili ni jambo la busara na mfano wa kuigwa,” amesema Mwampiki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Bombambili, Saidi George Kumbemba, amemshukuru Mbunge huyo kwa kuunga mkono jitihada za wananchi na wadau waliotoa michango katika ujenzi wa barabara hiyo inayokwenda kwenye makaburi ya Iyela, Jimbo la Mbeya Mjini.
Amesema msaada huo unaonyesha dhamira ya dhati ya Mbunge huyo katika kuunga mkono maendeleo ya wananchi pamoja na kuendelea kutatua changamoto za miundombinu katika mtaa huo.

Awali, Februari 2, 2026, wananchi wa Mtaa wa Bombambili katika Kata ya Mwakibete walifanya mkutano kujadili changamoto hiyo na kukubaliana kuanza kuchangisha michango ili kujenga barabara hiyo kwa nguvu zao wenyewe, baada ya kukumbana na ugumu mkubwa wa kufika katika shughuli mbalimbali za kijamii.

More Stories
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
Tanzania yaelekezwa kuongeza ushiriki katika biashara ya kaboni kimataifa.