Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya
MBUNGE wa Mbeya Mjini na Naibu Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amekabidhi mifuko 200 ya saruji kwa shule ya Sekondari Iganzo kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa ambavyo tayari wananchi walishaanza kuvijenga kutumia nguvu zao.
Baada ya kuguswa na changamoto kubwa ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa kutokana na ongezeko kubwa la ufaulu wa wanafunzi wanaotarajiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2021, Dkt.Tulia alitembelea shule hiyo ili kutoa mchango wake.
Amesema, pamoja na kukabidhi mifuko hiyo ya saruji pia ametoa ndoo 10 kwa ajili ya wanafunzi kunawia mikono ili waweze kujikinga na maradhi mbalimbali.
Hata hivyo Dkt. Tulia amesema kwamba, saruji hiyo itasaidia ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa ambavyo vinatakiwa kukamilika mapema ili mwakani watoto waweze kuanza masomo.
“Niwaombe ndugu zangu hii saruji isipotee hata mfuko mmoja ifanye kazi iliyokusudiwa,hapa tunahangaika ili watoto wetu waweze kusoma hivyo tuwe waaminifu ndugu zanguk,” amesema Dkt. Tulia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntika amesema kuwa, misaada itaendelea kupokelewa ila wananchi waendelee kuchangia nguvu kazi kama kawaida ns kuionya Kamati inayosimamia ujenzi kutothubutu kuchukua hata mfuko mmoja wa saruji na ikitokea imechukuliwa watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Mratibu wa Elimu kata ya Iganzo, Danstan Hepelwa amesema, walikuwa na watahiniwa 510 waliofanya mtihani wa darasa la saba na kati ya hao waliofaulu ni 435.
Amesema, kutokana na idadi kubwa ya ufaulu kuna upungufu wa vyumba vitano vya madarasa ambavyo vinatakiwa kujengwa ili mwakani watoto waweze kuanza kidato cha kwanza.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua