November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia atoa maelekezo kwa Jiji la Mbeya kwa waathirika Maporomoko ya tope Itezi

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

WAATHIRIKA wa mafuriko yaliyotokea April 14,2024 katika kata Itezi Jijini Mbeya wameiomba serikali kuwapatia maeneo mengine kwa ajili kujenga makazi kutokana na maeneo yaliyotengwa kutokuwa salama na kuwa ndani ya mita 60 eneo la hifadhi ya mto.

Mmoja wa wakazi wa kata ya Itezi ambaye ni mmoja wa waathirika hao ,Shadrack Elia amesema kuwa nje ya misaada waliyosaidiwa ,kwenye suala la viwanja uwezekano wa kujenga makazi ya kuishi ni mdogo kutokana na maeneo hayo kutofaa kwa makazi .

“Kwa hali za maisha yetu tulizonazo uwezekano wa kujenga ni ngumu kutokana na mazingira ya viwanja hivyo ,lakini pia kuhusu misaada ambayo tumekuwa tukipatiwa na serikali na wadau tunaomba kila mtu apewe chake kwani hivi sasa kuna wengine tayari wameanza kujiwekeza kwa maeneo ambayo yapo vizuri kwa ajili ya makazi kutokana na hali za maisha kutofautiana kwenye kipato “amesema Elias.

Mwafrika mwingine wa maporomoko hayo Nazareth Zabron ameiomba serikali iwasaidie kuwapatia maeneo ambayo yatakuwa jirani na huduma za kijamii na maeneo rafiki kulingana na uwezo wao wa kimaisha yao yalivyo .

“Haya maeneo ambayo baadhi yetu wamepatiwa si rafiki kabisa kwa makazi hivyo tunaomba serikali itusaidie kupata maeneo mazuri ambayo hayatakuwa changamoto kwetu na yataendana na hali zetu katika kujenga makazi yetu ya kudumu”amesema .

Frola Mwajibiri, ameshukuru kwa misaada mbalimbali lakini maeneo hayo yanaonekana kuwa changamoto kutokana na kuwa kwenye maporomoko na hakuna miundombinu ikiwemo Hospitali ,Shule hivyo kutofaa kwa makazi .

“Tunashukuru tumeonyeshwa maeneo tuliyopewa na serikali chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan lakini kuna changamoto kubwa kwetu ni ngumu kujenga makazi yetu ya kuishi tunaomba tu serikali itusaidie kutafuta maeneo mengine ambayo yatakuwa rafiki kwetu”amesema mkazi huyo kata ya Itezi .

Spika wa Bunge na Rais umoja wa Mabunge duniani ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya,Dkt.Tulia Ackson amewatoa hofu wananchi waliokubwa na maafa hayo kata ya Itezi ambapo amesema wananchi hao watambue kuwa serikali inawajali na kwamba viwanja walivyopatiwa sio kwamba kila sehemu ambako wanapata changamoto ya kama hizi wanapatiwa maeneo isipokuwa wao wamepatiwa kutokana na uzito wa tatizo lao.

“Leo tumekuja na majibu ya maeneo haya kuhusu hati nasema waliolipia hati watarejeshewa fedha zao na kupatiwa hati na ambao hawajalipia hati zitengenezwe kwa mujibu wa viwanja na wale watu watano ambao viwanja vyao vipo tayari na havina changamoto wakabidhiwe hati “amesema Dkt .Tulia.

Akielezea zaidi Dkt .Tulia amesema Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maagizo wananchi waliopatwa na maafa hayo wapewe viwanja kutokana na mazingira ya suala hilo lilivyojitokeza kwa wahanga hao wa maporomoko.

Ofisa Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya Declay Nyato amesema kuwa atafatilia kujiridhisha kama viwanja hivyo vipo ndani ya mita 60.

Dkt Tulia akiwa na Diwani wa Kata ya Itezi Sambwee Shitambala katika ofisi za kata hiyo ambapo Tulia alikuwa akisoma majina ya waathirika wa maporomoko ambao wanatakiwa kupatiwa viwanja na ambao viwanja vyao havina changamoto