January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Stergomena mgeni rasmi miaka 41 ya SUMAJKT

Na Penina Malundo,timesmajira, Online

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ,Dkt.Stergomena Tax anatarajia kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 41 ya kuanzisha kwa Shirika la uzalishaji mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT).

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT),Kanali Petro Ngata alisema maadhimisho hayo yanatarajia kufanyika sambamba na maonesho ya 46 ya biashara ya kimataifa Sabasaba katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema Shirika lao linajivunia kusherekea miaka 41 tangu kuanzishwa kwake kwani limeweza kufanikiwa kutimiza malengo ya uanzishwaji wake ikiwemo  kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli za JKT na kusaidia katika kujenga uchumi wa nchi.

”Maadhimisho haya tunatarajia kuanza Juni 29,mwaka huu na kilele chake kitakuwa Julai mosi,2022,kipindi chote shirika limeweza kufanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kibiashara na ile ya huduma yenye maslahi ya kitaifa ikiwemo ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa madini ya Tanzanite Mirerani mkoani Manyara na kujenga mji wa Kiserikali jijini Dodoma,”amesema 

Amesema pia  shirika lao limefanikiwa kuchangia pato la taifa kwa kutoa gawio Serikalini na kutoa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu mbalimbali.

”SUMAJKT limesaidia kutoa ajira kwa vijana wa kitanzania kupitia kampuni na miradi yake ikiwemo Kampuni ya Ulinzi SUMAJKT Guard hadi sasa imetoa ajira kwa vijana zaidi ya 16000,”amesema na kuongeza

”Shirika limekuwa likisaidia vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa kujifunza stadi za kazi kupitia shughuli zake mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo kilimo,ufugaji ,ujenzi,utengenezaji wa Samani na bidhaa za ngozi,”anesema