March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Shinhu:Wananchi wanauelewa mdogo utunzaji maji

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOline,Dodoma

MKURUGENZI wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria,Dkt.Renatus Shinhu amesema moja ya changamoto inayolikabili bonde hilo ni uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa maji unaopelekea uharibifu mabonde ya maji.

Shinhu ameeleza hayo leo jijini hapa leo Machi 6, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa miradi inayosimamiwa na bodi hiyo kwa mwaka 2025/2026 ambapo aliwataka wananchi kutambua kila mtu anajukumu la kutunza maji huku akisema maji ni rasilimali,maji ni uchumi na maji ni maisha.

Amesema endapo jamii itajengewa uelewa wa pamoja katika kusimamia rasilimali za maji ikiwemo vyanzo vya maji kutasaidia kuwa na vyanzo vya maji salama na endelevu.

“Tunahitaji kuwa na uelewa wa pamoja, kuhakikisha kwamba tunasimamia rasilimali za maji kwa maana ya mito, maziwa na vyanzo vingine ambavyo tuko navyo. Tunahitaji wananchi waweze kuwa na uelewa kama ambavyo tunaelewa sisi kwamba maji ni rasilimali adimu, maji ni uchumi, maji ni maisha, kwa hiyo tukishaelewa kwa pamoja maana yake inatusaidia sisi pamoja na wananchi kuweza kuhakikisha kwamba rasilimali za maji zinabaki kuwa endelevu,”amesema Shinhu.

Vilevile Shinhu amesema kuwa bodi yake imefanikiwa kukarabati na kujenga mabwawa mapya yaliyofikisha jumla ya mabwawa saba nchini. Ameongeza kuwa mabwawa hayo yanasaidia kuhifadhi maji ya mvua na kuyatumia wakati wa kiangazi, jambo linalosaidia kupunguza upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali.

Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 bodi imejenga mabwawa mawili katika Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu, ambayo ni Bwawa la Mashariki na Bwawa la Bugarama. Aidha amebainisha kuwa mabwawa hayo yanalenga kuimarisha upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu, kilimo, na mazingira ili kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa uendelevu.

‎”Ujenzi wa mabwawa ni sehemu ya jukumu la bodi la kuendeleza rasilimali za maji kwa kutafuta vyanzo vipya vya maji.Mabwawa haya yanasaidia kuvuna maji ya mvua badala ya kuruhusu maji hayo yatiririke na kupotea, hivyo kuwa chanzo kipya cha maji kinachoweza kutumika kwa muda mrefu,”amesema.

‎Pia, amesema kuwa bodi inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali ili kuimarisha usalama wa maji. Aidha amebainisha kuwa miradi hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa maji na kusaidia shughuli za kiuchumi na kijamii kama kilimo na viwanda.

‎Akizungumzia ugawaji wa maji (allocation), Shinhu ameeleza kuwa bodi imeendelea kutoa vibali vya matumizi ya maji kwa kuzingatia sheria na sera zilizopo.

Ambapo hadi sasa amesema zaidi ya vibali 1,396 vya matumizi ya maji vimetolewa katika maeneo tofauti, hatua inayosaidia kusimamia rasilimali hiyo kwa ufanisi.

‎”Ugawaji wa maji unafanyika kwa kuzingatia Sera ya Maji ya mwaka 2002 pamoja na toleo jipya la mwaka 2005. Sera na sheria hizo zinaelekeza namna bora ya kugawa maji ili kuhakikisha matumizi yake yanazingatia mahitaji ya binadamu, mazingira, na shughuli za kiuchumi,”amesema