December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Shelukindo akutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Vietnam, nchini Mhe. Nguyen Nam Tien katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, tarehe 9 Agosti 2023.

Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo maandalizi ya Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta za kipaumbele hususan utalii, kilimo, afya, TEHAMA, biashara na uwekezaji, uchumi wa buluu na maeneo mengine.

“Vietnam itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara wa Tanzania katika kuhakikisha wanapata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu wa kibiashara nchini Vietnam ili kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji,” amesema Balozi Tien.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Tien amesifu uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Viet Nam. Pia, ameeleza kuwa Vietnam inafurahishwa na Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Shelukindo amesema kwamba Tanzania inajivunia kuwa na uhusiano imara na Vietnam uliodumu kwa zaidi ya miaka 60.

Dkt. Shelukindo amezialika kampuni kutoka Vietnam kuja kuwekeza nchini katika miradi ya kimkakati kwa maslahi ya pande zote mbili. “Nawaalika wafanyabiashara na wewekezaji wa Vietnam kuja kuwekeza Tanzania kwa kuwa Serikali imeboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.” amesema Dkt. Shelukindo.

Dkt. Shelukindo ameongeza kuwa Vietnam imechangia vyema katika kukuza sekta ya mawasiliano kupitia Kampuni ya Halotel ambayo imetoa ajira kwa Watanzania.