Na David John Timesmajira online
RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan, amesema ni aibu kwa Bara la Afrika kuwa na vifo vya watu vinavyotokana na njaa au hata kutajwa kuwa na watu milioni 283, wanaolala na njaa kila siku.
Akizungumza katika Mkutano mkuu wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF), jijini Dar es Salaam, amesema inasikitisha kuona kwingineko Afrika, kuna watu wana utapiamlo na magonjwa mengine yanayotokana na lishe.
Rais Dkt. Samia amesema, kutokana na fursa zilizopo Afrika, ikiwemo asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani, asilimia 60 ya maziwa makuu duniani, asilimia 60 ya vijana duniani, Afrika haipaswi kuwa ilivyo sasa.
“Pamoja na baraka zote tulizobarikiwa, Afrika bado tumebaki kuwa walalamikaji, badala ya kutafuta njia za kuelekea katika mapinduzi ya kijani,” amesema katika hotuba yake ya ufunguzi wa majadiliano katika mkutano Jukwaa la Mifumo ya chakula Afrika.
Kadhalika, amesema kutokana na upekee wa bara la Afrika, viongozi wa mataifa yote wanatakiwa kutathimini vipaumbele vya nchi zao na kuzihusianisha na mahitaji ya sasa katika muktadha wa kidunia.
Amesema, AGRF ni moja kati ya majukwaa muhimu kwa Waafrika kutafuta suluhu ya changamoto zilizopo katika sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo ili hatimaye kuifikia Ajenda ya Afrika tiitakayo, yenye malengo hadi mwaka 2063.
Rais Dkt . Samia amesema, anatambua kuwa zipo ahadi kadhaa ambazo viongozi wameziweka kwa pamoja ili kufikia makubaliano mbalimbali ya kimataifa katika sekta ya kilimo ikiwemo kuongeza bajeti za kilimo na kutafuta ajira za vijana kupitia kilimo, lakini zinatakiwa kutimizwa kwa vitendo.
Katika mkutano huo, viongozi wa mataifa ya Afrika akiwemo Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt William Ruto walipata nafasi ya kuchangia maoni yao juu ya namna ya kufanya mnyoyoro wa thamani katika mifumo ya chakula Afrika AGRF inaboreshwa na kumaliza changamoto ya njaa barani Afrika.
More Stories
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi