December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Samia mgeni rasmi onesho la utalii SITE

Na Penina Malundo, timesmajira

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika onesho la utalii la Kimataifa la Swahili International Tourism Expo – SITE linalotarajia kufanyika Oktoba 6 hadi 8 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Maliasili na Utali, Angellah Kairuki, wakati akizungumza na waandishi wa habari na Wahariri kuhusiani na maandalizi ya mkutano huo ambao yatafanyoka Mlimani City.

Kairuki amesema maandalizi ya onyesho hilo yamekamilika na linatarajia kuwakutanisha wadau wa utalii kwa lengo la kufanya biashara na kushiriki semina mbalimbali, midahalo inayoangazia mada za utalii na fursa za uwekezaji.

“Katika kipindi chote limekuwa ni jukwaa muhimu lenye ushawishi kwa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi walio katika mnyororo wa huduma za utalii na mwaka huu SITE imewakutanisha mabalozi, bodi za utalii kutoka nchi za Afrika zikiwemo Uganda na Malawa, waonyeshaji (Exhibitors) zaidi ya 100 kutoka ndani na nje ya nchi,”amesema.

Kairuki amesema wanunuzi wa biashara za utalii zaidi ya 70 kutoka katika masoko yetu ya kimkakati ya kimataifa hususani Ulaya, Amerika na Asia.

Aidha, amesema kwa mwaka huu kutakuwa na bustani ya wanyama hai ili kuwavutia watembeleaji na kuhamasisha utalii wa ndani na Jukwaa la Uwekezaji la Utalii (TTIF).

Kairuki amesema wanyamapori hao ni simba dume na jike, chui, chatu, mbuni, nungunungu, kobe na aina mbalimbali ya ndege.

Aidha Waziri Kairuki ametoa rai kwa Watanzania, Wawekezaji na wadau wengine wa utalii kushiriki kikamilifu onyesho la SITE 2023, ambalo ni fursa ya muhimu kukutana ili kwa pamoja kuhakikisha sekta hiyo inapiga hatua.

“Tukitambua malengo makubwa tuliyonayo ni kufikia watali milioni 5 na mapato ya Dola za Kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025 na kuendelea kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia utambulisho wetu wa Tanzania,kupitia Unforgettable na program ya The Royal Tour,”amesema Waziri Kairuki