David John Timesmajira online
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan ameelezea hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali katika kutafuta masoko kwa ajili ya mazao ya wakulima hapa nchini.
Dkt Samia ameyasema hayo leo Septemba 7,2023 katika mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) wakati akijibu maswali kutoka Kwa wadau kwenye mkutano uliohusisha vijana ambapo ametumia nafasi hiyo kuelezea hatua wanazochukua kuondoa changamoto ya soko Kwa wakulima.
Akizungumzia changamoto za masoko amesema kuna shida katika kupatikana masoko lakini katika tafiti ambazo tumefanya tumegundua kuna mambo mawili ambayo yana utata na tunayafanyia kazi
“Jambo la kwanza ni Connection kwanza kujua mahitaji na balansi , balansi gani inatakiwa wapi ndani na nje ya nchi ,tukijua hilo tutakuwa na usahihi wa kinachozalishwa upande mmoja kiende upande mwingine,”amesema.
Amesema jambo la pili ni Connectio ya mkulima na soko lenyewe na kwamba eneo hilo hawajafanya vizuri bado huku akifafanua wameanza katika baadhi ya mazao kwa mfano korosho.
“Tumeshuhudia mara kadhaa bei ya korosho ikipanda kwasababu kuna ushirika wa mkulima na mnunuaji moja kwa moja, hivyo tumemuondoa mtu wa kati amba walikuwa wanakwenda moja kwa moja kununua mazao shambani na wananunua kwa bei ndogo.
“Tulivyounganisha mkulima na mnunuzi pamoja na soko wanunuaji wananunua kwenye vyama vya ushirika vya wakulima na kwa maana hiyo wanapata muda wa kushindana bei na bei zinapanda.
“Tumeshuhudia hivi karibuni zao la ufuta kwasababu tumeingiza kwenye ushirika na tumetumia mfumo wa stakabadhi ghalani, wakulima wanapeleka mazao yao huko kwenye ushirika , wanunuaji wanashindanishwa bei inapanda,”amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa “la kufurahisha zaidi ni katika zao la mbaazi ambalo miaka miwili, mitatu nyuma walihamasisha wakulima walime sana na wakalima lakini kwasababu hawakuwaunganisha na soko na hawakuwa na mipango mizuri mbaazi zilianguka bei sana na kuwavunja moyo wakulima
“Mwaka jana (2022) mbaazi iliuzwa kwa Sh.300 kwa kilo lakini mwaka huu(2023) wakulima wameuza kwa zaidi ya Sh.2000 kwa kilo. Sasa huu ndio mtindo tutakaokwenda nao kwenye mazao mengine pia ili kumuunganisha mkulima na soko,”amesema.
Akifafanua zaidi amesema hatua nyingine wanayochukua soko linahusu usafiri na usafiri ndio unaleta soko , hivyo Serikali ya Tanzania imejidhatiti kujenga barabara kuunganisha mikoa na mikoa , mikoa na wilaya zake lakini barabara kubwa na nchi jirani ili kufanikisha masoko ya nchi jirani
“Katika barabara mwaka jana na mwaka huu tumetoa fedha nyingi sana kutengeneza barabara za ndani ya wilaya ili mazao yasikwame kwa wakulima yaende kwenye masoko
“Lakini sio barabara peke yake tunatengeneza bandari zetu Tanzania , bandari ya Dar es Saalam, Zanzibar ,Tanga na Mtwara , zote ziweze kupokea meli zinazoweza kushusha na kuchukua mazao yetu yanayozalishwa kwenda nje na tumefanikiwa vizuri
“Pia kama mnavyoelewa tumenunua ndege ya mizigo ili isafirishe mazao hasa mazao ya matunda ambayo yanakaa kwa muda ambapo kwa ndege ile sasa tunaweza kuchukua mizigo yetu wenyewe na kuipeleka kwenye soko kuliko kutegemea kwa jirani apakie apelike
“Kwani hatujui wakati wa kupakia pengine mazao yale yale yameandikwa yametoka kwa jirani wakati yametoka Tanzania.Kwahiyo sasa ndege yetu itaweza kutusafirisha mazao yetu,”amesema.
Aidha amesema katika bandari wanajenga sehemu itakayoweza kuhifadhi mazao yanayoharibika kwa haraka yaweze kuhifadhiwa wakati yanasubiri usafiri.“Kwa hiyo tunachukua hatua zote hizi ili kumfikisha mkulima, kufikisha mazao kwenye soko.”
Pia amesema jambo lingine kubwa ambalo wanafanya hasa katika mpango wa BBT ni kutafuta na kufanya ushirika na watu ambao watakuwa wakiongeza thamani mazao ya vijana.
“Kwa maana vijana wakilima na wakivuna kuwe na mtu anayechukua mazao yote na kuyapeleka kuyaongeza thamani kwenye viwanda vyetu yakiwa yamechakatwa. Kwahiyo hizo ndizo hatua ambazo serikali inazichukua kuimarisha soko
Kuhusu Serikali kutumia ICT katika kilimo ili kuwavuta vijana kujikita kwenye sekta ya kilimo Rais Samia amesema kwa upande wa Tanzania hatua ambazo wanachukua kwanza ni kukubali katika karne tuliyonayo hizi ICT au taarifa za kutumia mitandao na teknolojia ya kisasa haiepukiki na inaweza kuingia kwenye sekta ya kilimo
Amesema ni lazima tuwatoe fikra vijana kwamba kulima ni kazi ngumu , kwa hiyo teknolojia inakwenda kurahisha kilimo kwa vijana
“Sasa Tanzania tumejua kilimo ni kujua taarifa zake na kwa maana hiyo tunawekeza sana katika tafiti na katika tafiti tunafanya maeneo yote kilimo,uvugaji na uvuvi .
“Katika kilimo tumejielekeza sana kwanza kujua afya ya udongo lakini kabla ya kujua afya ya udongo ni kuwa na kanzi data ili kuweza kufanya vizuri.
“Kwa hiyo kwa kutumia ICT tunaendelea kusajili wakulima ,aina ya kilimo wanachofanya, eneo walionalo na mambo mengine yanayomhusu mkulima.”
Ameongeza lakini ili mkulima huyo aweze kufanya vizuri lazima wajue mkulima yuko kwenye hali gani pale alipo, kwa hiyo wamewaazesha maofisa ugani vifaa vya kupima afya ya udongo ,
“Kwa hiyo kila mkulima atakuwa anapimiwa afya ya udongo kutoka muda mmoja kwenda mwingine na kujua kwa uhalisia anatakiwa kutumia mbegu za aina gani…
“Lakini tumejiingiza katika kuongeza uzalishaji wa mbegu za kisasa , tumeimarisha vituo vya utafiti na mashamba ya uzalishaji mbegu kwa kiwango kikubwa ili wazalishe mbegu sana.
“Kwa mfano Arusha kuna kampuni ya mtu binafsi lakini kuna na wengine nao wanazalisha mbegu.Vituo vyetu vya Serikali na vyenyewe tumeviwezesha na tunategemea ikifika mwaka 2025 labda robo tatu ya mbegu zitakazotumika kwa zizalishwe hapa nchini kama sio kujitegemea kabisa,”amesema Rais Samia.
Ameongeza na mbezu zinazozalishwa zinatambulika na zinaweza kuhimili mabadiliko ya hali ya hewa lakini zinaenda na hali ya udongo tulionao.
Aidha amesema wanatumia ICT katika masuala ya umwagiliaji kwani kama mnavyotambua zamani wakisema umwagiliaji ilikuwa ni umwagilia haswa kwa maana ya kuchukua maji na kuyamwaga katika udongo ili mazao yaje kama inavyomwaga mvua.
“Sasa tunamwagilia kwa kutumia teknolojia ya kitalaam ambayo mti humwagiliwa kwa maji yanayotakiwa na muda unaotakiwa.Lakini pia kujua aina ya udongo ulionao unahitaji maji kiasi hiki na sio kiasi hiki na hiyo itasaidia kufanya matumizi mazuri ya maji tuliyonayo.
“Pia tunakwenda kutumia ICT katika kuhifadhi mazao ya wakulima , tunajenga vihenge vya kisasa ambavyo vinamitambo ya kurekebisha mvuke na kuepusha tatizo la kuwa na sumu kuvu katika mazao yetu, tunakwenda kufanya hivyo kwa kutumia ICT.
“Kwa hiyo tunakwenda kutumia ICT kwenye soko kwani lazima tujue taarifa za mahitaji ya matwaka na ugavi wa mazao yanayozalishwa ndani ya nchi.Hivyo ICT haiepukiki , lakini hata teknolojia katika kutayarisha mashamba na tunahitaji kuwa na mitambo ya kisasa na ndio itakayotumika katika mpango wa BBT.”
Amesema ni lazima kijana ajisikie fahari anaendesha trekta ambalo ni la kisasa na linafanya kazi zaidi ya moja.”Kwa hiyo ICT haiepukuki na Serikali yetu tumedhamiria kuelekea huko.
Matokeo ya mpango wa BBT
Rais Samia amesema viashiria vya kufahamu kwamba mpango huo umefanikiwa kwanza ni idadi ya vijana walio katika mpango huo ambao wapo zaidi ya 1200 lakini bado kuna maombi mengi kutoka kwa vijana kutaka kuingia katika huo mpango.
Amesema kwa hiyo kiashiria cha kwanza ni vijana kuvutika na mpango wa BBT , lakini kiashiria cha pili kitakuwa kwa namna wanavyotumia mbolea katika kuzalisha , jinsi inavyotumika sana ndipo watajua vijana wameelewa na wanafanya kilimo cha kisasa.
“Kwa hiyo matumizi ya mbolea itatupa kiashiria kwamba kuna matokeo chanya lakini tatu ni tija itakayopatikana katika kile ambacho vijana watakuwa wamehusika nacho,”amesema.
Pia amesema kiashiria kingine ni soko kwa maana ya jinsi vijana watakavyopeleka hayo mazao sokoni na watakavyoendesha maisha yao.Hivyo , ndio viashiria lakini kikubwa zaidi ni kuona maisha ya vijana yanavyoendelea kustawi,
Amesema kiashiria kingine cha kufanikiwa kwa mpango wa BBT ni kuona wameshusha mfumuko wa bei ya gharama za chakula ndani ya nchi.
“Kama uzalishaji utakuwa mkubwa bila shaka bei za chakula zitashuka na kama tunavyojua mfumuko ndio unasababisha bei za chakula kupanda ndani ya nchi.
“Tukiweza kushusha mfumuko wa bei ya vyakula kitakuwa kiashiria kizuri sana kwamba vijana wanazalisha kwa wingi.”
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa