November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Philip atoa wito kwa nchi wanachama Zisizofungamana na Upande Wowote

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa nchi wanachama Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement) kuendelea kufanya kazi kwa pamoja na mshikamano katika kutumia fursa , kukuza biashara ya kimataifa na uwekezaji, kushirikishana mbinu bora na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 02 Machi 2023 wakati akihutubia Mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non- Aligned Movement) uliolenga kujadili namna ya kukabiliana na athari za Uviko-19 uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Baku nchini Azerbaijan.

Makamu wa Rais amesema Janga la Uviko-19 limetoa somo la kutotegemea msaada wakati wote hivyo inapaswa nchi wanachama kuwekeza katika tafiti na maendeleo kwa ajili ya kutatua changamoto za ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na bioteknolojia,utengenezaji wa chanjo, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa nyinginezo za kuokoa Maisha ya wananchi.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito kwa mataifa wanachama kuhakikisha yanaimarisha uwezo katika ufuatiliaji ili kutambua kwa wakati na kuzuia magonjwa ya kuambukiza kwa manufaa ya afya ya umma kwa kujumuisha ujenzi wa miundombinu, mifumo thabiti ya afya na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya ili kudhibiti milipuko. Ameongeza kwamba ni muhimu kuimarisha lishe bora na ustawi wa kimwili wa wananchi ambao ni muhimu kwa maisha yenye afya na ustahimilivu wa magonjwa.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito wa ushirikiano wa kina baina ya mataifa yanayoendelea pamoja na kuimarisha uhusiano wa nchi zilizoendelea na zinazoendelea kwa misingi ya kuheshimiana kwa maslahi ya ustawi wa pamoja. Amesema Tanzania inaendelea kutoa wito wa kukomeshwa kwa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na mataifa makubwa kwa Jamhuri ya Cuba na Jamhuri ya Zimbabwe.

Akitoa uzoefu wa Tanzania katika kukabiliana na athari Uviko 19 , Makamu wa Rais amesema serikali ilihamasisha utoaji chanjo na kusambaza chanjo kwa walengwa ambayo ilisaidia katika kudhibiti janga hilo, kuongeza miundombinu ya kutolea huduma za afya pamoja na kuongeza watoa huduma, vifaa tiba na dawa muhimu. Makamu wa Rais ameshukuru Jumuiya yab nchi Zisizofungamana na Upande Wowote kwa sauti iliyowezesha kupokea chanjo zinazohitajika wakati wa janga hilo.

Pia ametaja hatua zingine zilizochukulia ikiwa ni pamoja na kutumia mkopo wa masharti nafuu chini ya dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), ili kuongeza uwezo wa miundombinu katika elimu, afya na maji ili kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na kutoa msaada kwa sekta zilizoathirika zaidi ikiwa ni pamoja na utalii, viwanda na biashara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Rais wa Azerbaijan Mheshimiwa Ilham Aliyev wakati alipowasili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Baku nchini Azerbaijan kuhudhuria Mkutano wa nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement) leo tarehe 02 Machi 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia katika Mkutano wa nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (Non-Aligned Movement) uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Baku nchini Azerbaijan leo tarehe 02 Machi 2023