November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Noel Lwoga miongoni mwa wakurugenzi bora 100 Tanzanzia 2022

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dr Noel Lwoga ni miongoni mwa wakurugenzi bora 100 Tanzania kwa mwaka 2022 ambao walipewa tuzo zao jana 27 Novemba 2022.

Ushindi huo ni kulingana na uchambuzi uliofanywa na Kampuni ya Easternstar kwa kushirikiana na Taasisi ya Mameneja Tanzania (Tanzania Institute of Managers) na kampuni nguli ya kimataifa ya uchambuzi ya KPMG.

Aidha, Dkt. Noel Lwoga amekuwa mshindi wa tatu katika kundi la viongozi wa taasisi na mashirika ya Serikali sita zilizoingizwa kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wakurugenzi wengine walizoingia kwenye kinyaganyiro hicho ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Hosea Kishimba ambaye ndiye alikuwa mshindi wa kwanza kwenye kundi hilo na Dkt Evance Mwasse, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Serikali la Madini (STAMICO).

Wengine ni Ladislaus Matindi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Fred Msemwa, Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing Investment na Godfrey Nyaisa, Mkurugenzi Mkuu wa BRELA.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga amewashukuru waandaaji na waratibu wa zoezi hilo kumpendekeza kuwa sehemu ya washindi.

Aidha, amesema tuzo hiyo ni kazi na juhudi kubwa inayofanywa na timu ya viongozi na wafanyakazi wa Makumbusho ya Taifa kwa ujumla.Mgeni rasmi katika ghafla ya utoaji tuzo hizo alikuwa Omary Shabani, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar ambaye aliwapongeza washindi wote na kuwataka waendelee kufanyakazi kwa weledi kwa manufaa ya taasisi zao na taifa kwa ujumla.

“Kutambulika huku kuwe kichocheo cha kuendelea kufanyakazi kwa uadilifu na weledi zaidi ili muwe mfano kwa wale wanaowaongoza” alisema Mhe. Naibu Waziri.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Mameneja Tanzania Deo Kilawe amesema kuwa taasisi yake ilianzisha kazi ya kutambua viongozi wanaofanya vizuri kwa sababu ya kujua kuwa uadilifu katika kazi ni jambo muhimu ambalo linatakiwa kufuatwa na kila mtumishi.

“Tulitafuta taasisi inayoaminika ili kuchambua wakurugenzi bora kwa mwaka 2022 bila kuleta malalamiko kwa jamii na KMPG wamefanyakazi hiyo kwa weledi mkubwa,” amesema Bw, Kilawe.

Dkt. Noel Lwoga akiwa ameshirikilia tuzo aliyopokea baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika kundi la Wakurugenzi wa Taasisi na Mashirika ya Serikali.
Dkt. Noel Lwoga, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF baada wote kupokea tuzo za wakurugenzi bora kwa mwaka 2022
.
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga (kulia) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa CRDB DKt Abdulmajid Nsekela baada ya kupokea tuzo ya wakurugenzi bora wa mwaka 2022.
Dkt. Noel Lwoga akipokea tuzo ya Mkurugenzi bora nafasi ya tatu kwa kundi la taasisi za Serikali kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya KPMG, BW. Alex Njombe.