Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro ameagiza kuzingatia kwa matumizi sahihi ya fedha kwa maslahi ya taifa katika ujenzi wa mradi wa kituo jumuishi cha taasisi ya sheria kinachojengwa wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Dkt.Ndumbaro ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwenye jengo la kituo jumuishi cha taasisi za kisheria, iliofanyika Jana mkoani Mwanza.
Ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unapaswa kuwa kichocheo kwa ujenzi wa majengo mengine kama hayo nchini, ili kuweza kufikia malengo ni lazima wahakikishe wanatembea katika dira na dhima ya wizara hiyo.
Pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu na kuhakikisha uapatikanaji wa haki unakuwa rahisi kwa kila mtu.
“Kutokana na hili nipende kutoa shukrani Kwa serikali ya awamu ya sita,ambayo imeendelea kutoa fedha kwa mahakama ambapo miradi mbalimbali imeendelea kujengwa ikiwemo ujenzi wa vituo jumuishi katika mikoa mbalimbali nchini,”ameeleza Dkt. Ndumbaro.
Sanjari na hayo amemuhimiza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha kwa wakati jengo hilo kwa ubora kwani fedha zinazotumika ni za wananchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Feleshi ameeleza kuwa ujenzi wa vituo jumuishi utasaidia kuwezesha taasisi za kisheria za serikali, Wizara pamoja na wadau muhimu Kwa pamoja kuongeza tija katika kutoa huduma.
Dkt.Feleshi ameeleza kuwa mpango huo utafanikisha kazi zinazofanywa na mahakama mtandaoni pamoja na kuondoa changamoto zinazowakabili katika maeneo yenye mahakimu wengi kuliko mawakili wa serikali.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho Mkurugenzi wa Huduma za Ushauri kutoka Wakala Majengo Tanzania (TBA), Wencelaus Kizaba ameeleza kuwa jengo hilo litagharimu bilioni 3,(3,181,548,096.83)hadi kukamilika kwa ujenzi huo.
Kizaba ameeleza kuwa ujenzi wa jengo hilo ulianza Aprili 26 mwaka huu na unatarajia kukamilika Oktoba 25,2023 mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 35 wa kazi zote za mkataba.
Ameeleza kuwa mradi huo umetoa ajira mbalimbali kwa wataalamu na wafanyabiashara wadogo wadogo pamoja na mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo nchini.
“Vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi huu vinatoka kwenye viwanda vyetu vya ndani ikiwemo saruji,rangi,mabomba huku baadhi vitatoka kwenye viwanda vya nje,”ameeleza Kizaba.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima, ameeleza kuwa watashirikiana na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mbunge wa jimbo la Nyamagana,Florah Magabe ameipongeza Serikali kwa kuanzisha vituo jumuishi vitakavyosaidia kukabiliana na vishoka.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa